Ulinzi Youth inalenga makubwa Chapa Dimba
NA JOHN KIMWERE
LISILOKUWAPO moyoni, pia machoni halipo. Ni msemo unaoashiria kwamba hakuna linaloweza kutimia bila ya kufanyiwa kazi. Aidha unahimiza mhusika kuwa na mikakati mwafaka bila kuweka katika kaburi la sahau azimio analopania kufikia.
Ingawa ndiyo mwanzo kwa timu ya Ulinzi Youth kufuzu kushiriki fainali za kitaifa kuwania ubingwa wa Chapa Dimba na Safaricom imetangaza kuwa katu haina lingine ila inataka kubeba kombe hilo msimu huu. Akifunguka hayo kocha wake, Vincent Otieno amesema kwamba ana imani tosha kikosi chake kinatosha mboga kuvuruga wapinzani wao na kutwaa taji la muhula huu.
Ulinzi Youth itashiriki kinyang’anyiro cha msimu huu baada ya kutangazwa mabingwa wa taji hilo katika Mkoa wa Kati kwenye fainali za makala ya tatu (Season Three) zilizochezewa Uwanjani Nanyuki mwishoni mwa mwaka uliyopita.
”Ufanisi wa chipukizi wangu ulikuja kinyume na matarajio ya wengi hasa wapinzani wetu maana ndio uliokuwa mwanzo kwetu kushiriki michuano hiyo,” amesema kocha huyo na kuongeza kuwa anaamini mechi za fainali hazitakuwa rahisi.
FAINALI
Ulinzi Youth ilijikatia tiketi ya fainali ilipochoma JYSA FC magoli 3-1. Licha ya JYSA kutangulia kufunga kupitia Clinton Sheitara dakika ya tisa iliangukia pua baada ya wenzao kuzinduka na kuwazidi maarifa. Brian Kafero alisawazishia Ulinzi dakika ya 20 kabla ya Emmanuel Lenkai na Kelvin Akmat kutikisa wavu mara moja kila mmoja dakika ya 34 na 72 mtawalia.
”Kama ilivyo ada yangu huchukua dakika za mwanzo kusoma jinsi wapinzani wetu wanavyogaragaza gozi ya ng’ombe kisha kukipanga kikosi changu propa,” alisema kocha huyo wa Ulinzi Youth na kuongeza kuwa wamepania kuwasha moto mkali katika kipute hicho.
KUPIGWA STOPU
Fainali za kitaifa zilizokuwa zimeratibiwa kuandaliwa mwezi Juni mwaka huu Mjini Mombasa zilihairishwa kufuatia janga la korona ambalo limechangia shughuli nyingi kote duniani kukwama. JYSA ya Juja ilisajili ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya Irigiro FC ya Maragua nao wavulana wa Kimatugu kutoka Kirinyaga walinyukwa bao 1-0 na Ulinzi Youth lililotupiwa kimiani na Brian Kafero.
Ulinzi Youth ilionekana kufana zaidi ilipobeba tuzo tatu za kibinafsi ambapo Brian Kafero aliibuka mfungaji bora alipocheka na wavu mara mbili. Naye Elijah Mambo alituzwa mnyakaji bora huku tuzo ya mchezaji anayeimarika ikimwendea Kelvin Akmat.
TIMU SITA
Ingawa zimesalia fainali za maeneo mawili: Mkoa wa Magharibi na Nyanza tayari timu sita zimejikatia tiketi za kushiriki ngarambe ya kitaifa zitakaochezewa mjini Mombasa. Orodha ya vikosi hivyo inajumuisha: Laiser Hill Academy (Mkoa wa Bonde la Ufa), Berlin FC (Mkoa Kaskazini Mashariki), Ulinzi Youth (Mkoa wa Kati), Dagoretti Mixed (Mkoa wa Nairobi), Tumaini School (Mkoa wa Mashariki) na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa.