Michezo

Una wazimu? Wewe mpumbavu tu, kidosho amfokea Bendtner

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KIPUSA Philine Roepstorff ambaye kwa sasa anachumbiana na Nicklas Bendtner amemtaja mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal kuwa “mpumbavu mkosa akili” na “wazimu mkubwa” kutokana na mipango yake ya kutaka kujinunulia gari la kifahari la Rolls-Royce lenye thamani ya Sh42 milioni wakati ambapo hana kazi.

Bendtner ambaye ni mzawa wa Denmark, hajakuwa na klabu tangu Disemba 2019 baada ya kikosi cha nyumbani kwao cha FC Coppenhagen kilipomfurusha kwa matokeo duni.

Licha ya kusutwa pakubwa na mchumba wake, sogora huyo mwenye umri wa miaka 32 hakukatiza mipango ya kufunga safari ya kuelekea Ujerumani kufanikisha mipango ya kujinunulia gari jeusi aina ya Rolls-Royce Badge Wraith.

Bendtner ambaye aliwawajibikia Arsenal kwa kipindi cha miaka tisa kwa sasa hualikwa mara kwa mara kuchangia mijadala kuhusiana na soka na masuala ya mapenzi katika kimojawapo cha vipindi vinavyoendeshwa na mchumba wake kwenye Danish TV.

“Philine anahisi kwamba mpango nilionao wa kununua gari la kifahari ni sawa na wa mtu asiyetumia ubongo. Namuelewa kwa kuwa gharama yenyewe ni ya juu sana. Lakini asichokifahamu ni kwamba ni lazima mtu ajinyime mengi na apitie uchungu fulani ili azitimize nyingi za ndoto zake za maisha,” akatanguliza.

“Kingine ambacho mpenzi wangu haelewi ni kwamba pesa ninazotumia kujinunulia vitu nivipendavyo ni zangu na niko huru kuzitumia nitakavyo. Fedha ambazo nilitumia jasho jingi kujipatia bila yeye kuhusika kwa vyovyote,” akasema.

Kwa upande wake, Philine alisisitiza kwamba, “Bendtner anastahili kuelewa kwamba kwa sasa hana kazi. Gari analopanga kununua ni la kiwango cha juu zaidi ambalo nahofia kwamba litamshinda kulitunza ipasavyo, Isitoshe, ni gari ambalo hakuna mtu yeyote mwingine analimiliki nchini Denmark,” akasema kipusa huyo.

“Huwa na kiu ya kutaka kumiliki vitu ambavyo watu wengine nchini mwake hawana. Nimejaribu kumfinyanga bila ya mafanikio. Kwa sasa sina jingine la kusema kumhusu. NI mtu asiyeshawishika kirahisi kubadilisha msimamo, asiyeona uhalisia wa mambo, mpumbavu na wazimu,” akasisitiza.

Hadi alipobanduka kambini mwa Arsenal mnamo 2014, Bendtner ambaye pia amewahi kuchezea Birmingham, Sunderland, Nottingham Forest, Juventus, Wolfsburg na Rosenborg alikuwa amepachika wavuni mabao 45 kutokana na mechi 171 chini ya mkufunzi Arsene Wenger.

Mnamo Mei 2020, Bendtner alikiri kwamba aliwahi kupoteza kima cha Sh700 milioni kwa mchezo wa karata ya pata-potea akiwa na umri wa miaka 19.

Aidha, aliungama kuwa alikuwa akitumia asilimia kubwa ya mshahara aliokuwa akipokezwa na Arsenal katika kushiriki mchezo wa kamari uitwao Texas Hold’Em.