Unai ndiye asili ya masaibu Arsenal – Nyota
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Arsenal, Charlie Nicholas amesema shida zinazokabili klabu hiyo zilichangiwa na kocha Unai Emery ambaye alishindwa kusajili mabeki wazuri licha ya kutumia pesa nyingi katika soko la usajili la majira ya kiangazi, mwaka 2019.
Nyota huyo mstaafu ambaye pia aliwahi kuchezea klabu za Celtic, Aberdeen na Clyde alisema huenda hali hiyo ikawalazimu wakuu wa klabu hiyo kufanya maamuzi kabla ya kumalizika kwa msimu huu, hasa iwapo kocha huyo atashindwa kuandikisha matokeo mazuri katika mechi zijazo.
Katika mechi hizo, Arsenal imepangiwa kucheza na Southampton, Eintracht Frankfurt, Norwich City, Brington, West Ham United na Standard Liege.
Mbali na raia huyo wa Scotland, kiungo Henrikh Mkhitaryan anayechezea klabu ya AS Roma ni miongoni mwa watu wanaokosoa mbinu za Emery huku akidai kwamba mbinu zake haziwezi kuisaidia timu hiyo inayoshikili nafasi ya sita jedwalini, ikiwa imeachwa pointi 17 na Liverpool wanaongoza msimamo huo huo wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Kati ya mechi 12 za ligi hiyo msimu huu, Arsenal wameshinda nne, wakatoka sare tano na kushindwa mata tatu, matokeo ambayo yanaiwaweka katika hali ngumu kwenye vita vya kuwania kumaliza ndani ya nne za kwanza.
Mkhitaryan alisema kilichomfanya aondoke Arsenal ni tabia za Emery ambaye mara kwa mara alikuwa akimlazimisha kucheza kama winga, huku akimuongezea jukumu la kusaidia safu ya ulinzi.
“Nilikuwa ninaanza kama mshambuliaji wa pembeni lakini pia nikiwa na jukumu jingine la kusaidia kiungo wa ulinzi, kitu ambacho kilinizuia kufunga mabao mengi wala kuwapa wenzangu pasi za kufunga mabao,” alisema Mkhitaryan.
Kiungo huru
Alisema yeye hupenda kucheza kama kiungo huru, lakini ilikuwa vigumu kufanya hivyo kutokana na vile Emery alivyokuwa akimpanga.
“Nilikuwa mchezaji muhimu kikosini lakini niliamua kuodoka baada ya kushindwa kuelewa mbinu za Emery. Kadhalika Roma walitoa ofa nzuri ambayo ilinivutia. Kwa sasa nina umri wa miaka 30 na sitaki kukalia benchi na kupoteza muda wangu,” alisisitiza raia huyo wa Armenia.
Kikosini Roma, Mkhitaryan ni tegemeo katika wa timu hiyo akiwa amefunga mabao mawili katika Ligi Kuu ya Serie A mbali na kuwaandalia wenzake pasi kadhaa.
Baada ya kucheza mechi zilizotajwa hapo awali, Arsenal itakuwa na ratiba ngumu ndani ya siku 17 ambapo itakutana na Manchester City, Chelsea, Everton na Manchester United.
Kulingana na ripoti za klabu hiyo ya Emirates, kocha huyo wa zamani wa Sevilla na PSG amepewa mwezi mmoja kunusuru kazi yake.