Ureno na Uhispania bado ni nguvu sawa
Na MASHIRIKA
NYOTA Cristiano Ronaldo na Renato Sanches wa timu ya taifa ya Ureno, walishuhudia makombora yao yakigonga mwamba wa lango la Uhispania katika mchuano wa kirafiki uliokamilika kwa sare tasa mnamo Oktoba 7, 2020.
Uhispania walitamalaki mchuano huo katika vipindi vyote viwili huku wakipoteza nafasi nyingi za wazi zilizopatikana kupitia kwa Dani Olmo na sajili mpya wa Leeds United, Moreno Rodrigo.
Mechi hiyo ilichezewa mbele ya mashabiki 2,500 waliokubaliwa kuingia katika uwanja wa Jose Alvalade ulio na uwezo wa kubeba jumla ya mashabiki 50,000.
Kwa kawaida, uga huo hutumiwa na klabu ya Sporting Lisbon ya Ligi Kuu ya Ureno kuandalia mechi zake za nyumbani.
Ureno na Uhispania walikuwa wakivaana kwa mara ya kwanza tangu walipoambulia sare ya 3-3 kwenye mojawapo ya mechi za fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi. Wakati huo, mabao yote ya Ureno yalifumwa wavuni na Ronaldo ambaye ni fowadi matata wa Juventus.
Mechi ya Oktoba 7 ilikuwa ya kwanza kwa fowadi wa Wolves ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Adam Traore, kuchezea Uhispania.
Nusura ushirikiano mkubwa kati yake na Olmo mwishoni mwa kipindi cha pili uwape Uhispania bao la ushindi ila fataki yake ikadhibitiwa vilivyo na kipa Rui Patricio.
Kipa Kepa Arrizabalaga wa Chelsea alilazimika pia kufanya kazi ya ziada ili kumnyima fowadi wa Atletico Madrid, Joao Felix nafasi ya wazi ambayo vinginevyo, ingaliwapa Ureno bao mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Mechi hiyo ilikuwa ya 173 kwa beki na nahodha wa Uhispania, Sergio Ramos kuwajibishwa na timu yake ya taifa.