Ushindi kwa Thika Queens na Trans Nzoia Falcons
NA JOHN KIMWERE
TIMU za wanawake za Thika Queens na Trans Nzoia Falcons zilivuna mabao 7-1 kila moja dhidi ya Wadadia LG na Vihiga Leeds mtawalia kwenye mechi za soka ya Ligi Kuu msimu huu.
Katika uwanja wa Thika Stadium, malkia wa zamani Thika Queens ilitembeza ubabe wake na kuandikisha ufanisi wa pili baada ya kutandika Makolanders mabao 4-3 wiki iliyopita.
Warembo hao wa kocha, Benta Achieng walionyesha soka safi na kuzoa alama zote muhimu kupitia juhudi za Catherine Wangechi na Rachael Mwema waliopiga mbili kila mmoja, nao Fauzia Omar, Lucy Khumba na Mwanahalima Adams kila mmoja aliitingia bao moja.
”Bila shaka nashukuru wachezaji wangu kwa kuonyesha mchezo mzuri maana tunalenga kujitahidi kukabili wapinzani angalau kubeba taji la msimu huu,” mwenyekiti wa Thika Queens Fredrick Chege alisema. Naye Mercy Anyango alisawazishia Wadadia LG ambayo hunolewa na kocha Rashid Sumba.
Nacho kikikosi cha Trans Nzoia Falcons kilitandika wapinzani wao kupitia juhudi zake Martha Karani aliyepiga Hat trick, Sharo Mato aliyechapa mbili safi, nao Susan Muhonja na Valentine kila mmoja aliifungia bao moja huku Vihiga Leeds ikisawazisha kupitia Velma Isambo. Trans Nzoia Falcons ilishinda mchezo wa pili na kutwaa uongozi wa kipute hicho kwa kuzoa pointi sita sawa na Thika Queens zikitofautishwa na idadi ya magoli ya ushindi.
Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, kwa mara ya pili mfululizo Eldoret Falcons ya kocha Njoki Mutua ilidondosha mchezo wa pili ilipokubali kulala kwa mabao 4-1 mbele ya Kisumu Allstars baada ya Mary Airo na Bertha Adhiambo kutikisa nyavu mara mbili kila mmoja. Bao la kufuta la Eldoret Falcons lilifumwa na Ruth Ingosi. Nayo Kayole Starlets ilijikuta njia panda iliporandwa mabao 4-0 na Oserian Ladies.