• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
Usitarajie kuwaona ‘walimu’ wanaomfikia Alex Fergusson

Usitarajie kuwaona ‘walimu’ wanaomfikia Alex Fergusson

NA JOB MOKAYA

Enzi za makocha kuheshimiwa na kuogopwa Ulaya huenda sasa ndipo zimefika ukomo. Zama za timu kutetemesha wapinzani na makocha kuabudiwa zimetupa kisogo na kuwa ‘zilizopendwa’.

Nchini Uingereza makocha wawili waliotesa na kutetesha zaidi ni Sir Alex Fergusson aliyeiongoza Manchester United naye Jose Mourinho, aliyeiongoza Chelsea. Hawa wote wawili ni zilizopendwa sasa.

Alex Ferson alikwishastaafu na sasa ni ndugu mtazamaji. Naye Jose Mourinho kapigwa kalamu kwa msururu wa matokeo hafifu pamoja na mizozo ya mara kwa mara na wasakata-gozi. Huyu Mourinho akiogopwa sana na kila mtu kwa mbinu zake za soka.

Jose Mourinho, alijulikana kwa kushinda mechi nyingi licha ya kwamba mchezo wenyewe ulikuwa hafifu sana.

Mashabiki wa timu ya Mourinho wangepachika vitanga vya mikono yao kwenye upande wa kushoto wa kifua palipo na moyo.

Uwanjani, timu ya Mourinho ambayo ingekuwa kifua mbele bao moja kwa nunge, ingehami bao hilo moja huku wachezaji wengine wote wakiwa mbele ya golikipa wao kulinda bao hilo moja. Aghalabu, mechi hiyo ingeisha vivo hivyo kwa Mourinho moja, mpinzani yai.

Mfumo huu wa Mourinho, ndio uliozalisha madifenda wengi hodari pamoja na viungo wakabaji kama vile Mouraine Fellaini, Claude Makelele, Michael Esien, John Terry, pamoja na wafungaji hodari wa kushtukiza kama vile Didier Drogba, Arjen Robben na wengine kama hao.

Lakini mbinu zake zilihitaji wachezaji kujitolea na kujituma sana uwanjani.

Wale waliolalamika wangezomewa mbele ya kamera za runinga na picha hizo kupeperushwa kote duniani huku mchezaji akipatwa na aibu kuu asijue ajifiche wapi.

Leo hii, wachezaji wa kisasa hawatakubali kupawa aibu na kukimya kama mabubu mazuzu. Hao sio kina Paul Pogba na Anthony Martial.

Na inaelekea lawana za wachezaji zinasikizwa sana na mabodi ya usimamizi wa vilabu. Ndiyo maana Paul Pogba kamtimua Mourinho naye Mourinho kabaki kuchanganua tu soka ya timu nyingine.

Nayo Chelsea imebaki ikiwafanyia majaribio makocha wengi na kuwatimua pindi matokeo yawapo finyu. Kwa upande wake, Ferguson alitoka Manchester United na kuacha nyuma demu, yaani, nguo iliyochakaa.

United ikiendelea kucheza mchezo ambao hauna tofauti kubwa na timu ya Shabana kutoka Kisii, inayocheza katika daraja ya pili ya ligi ya Kenya.

Hata vijana wa K’Ogalo au Ingwe, wanaweza wakaitoa Man United kijasho nayo Tusker kuipenga kamasi.

Uhispania, Real Madrid na Barcelona si miamba tena. Zamani, Barcelona ikicheza mpira wa kutandaza sakafu kana kwamba ni programu ya tarakilishi. Ila siku hizi, wanacheza mpira hafifu kweli na kupoteza mara kwa mara.

Real Madrid nayo imekuwa kichekesho kingine. Timu ambayo imeshinda mataji mengi ya Champions League na kuwa na wachezaji hodari kuwahi kucheza soka kama vile Cristiano Ronaldo, Ronaldo yule wa Brazil, Zinedine Zidane -kocha wa sasa, na kipa Ike Carsilas, sasa inacheza soka ya kubahatisha.

Huenda hiki ni kipindi cha kudidimia kwa ukocha mzuri kwani kwanzia Uingereza ambapo ni Manchester City na Liverpool pekee wanaonawiri, hadi Ujerumani ambapo Bayern wanaona kivumbi, hata Ufaranza ambapo Monaco wamekuwa hovyo na ovyo na Italia ambapo San Siro ya AC Milan imekuwa uwanja wa mbuvi, ubora wa makocha na timu umeenda likizo.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: KEBS ibaini hatari kwa muda ufaao

SHANGAZI: Mke wa mpenzi wangu ananitishia maisha, nifanyeje?

adminleo