Uzbekistan yalipiza kisasi dhidi ya Kenya mechi ya kirafiki
Na GEOFFREY ANENE
WENYEJI Uzbekistan Jumatatu jioni walilipiza kisasi dhidi ya wageni wao Kenya katika mechi ya kirafiki ya timu za Olimpiki za mataifa haya uwanjani Istiqol mjini Fergana.
Emerging Stars ya kocha Francis Kimanzi ililemea vijana wa mkufunzi Ravshan Haydarov 2-1 katika mechi ya kwanza ya kirafiki Machi 23 uwanjani Avlod mjini Andijan, Uzbekistan iliizima Kenya 1-0, bao lililofungwa katika dakika ya 90+8.
Jumatatu alasiri timu hiyo ilikuwa imeapa kujitahidi kuigaragaza Kenya na kuepuka kichapo kingine. Lakini kikawa kibarua hadi dakika ya 90 ambapo matokeo bado yalisalia 0-0.
“Leo, timu yetu ya Olimpiki itateremka uwanjani kulipiza kisasi dhidi ya Kenya,” Shirikisho la Soka la Uzbekistan (UFF) lilisema.
Kabla ya mchuano huu, Kenya imepata kuonja hali ya uwanja wa Istiqol mapema Jumatatu kabla ya mechi ya marudiano dhidi ya mabingwa hawa wa Bara Asia. Uwanja huu unabeba mashabiki 20, 000.
Katika mechi iliyopita, Kenya ilitangulia kuona lango kupitia kiungo wa KCB Chrispinus Onyango na kumaliza kipindi cha kwanza mabao 2-0 juu baada ya mvamizi wa Wazito, Pistone Mutamba kufuma wavuni bao la pili.
Uzbekistan ilipoteza penalti katika kipindi cha pili kipa Timothy Odhiambo wa Ulinzi Stars alipopangua shuti la Zabihullo Urinboev dakika ya 72. Andrey Sidorov alifungia wenyeji bao la kufuta machozi sekunde chache baadaye.
Timu ya Kenya ilijiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki Olimpiki mwaka 2020 jijini Tokyo, Japan. Mbali na kuandaa timu yake ya Olimpiki, Uzbekistan pia inatumia michuano hii kujipiga msasa kwa mashindano ya Bara Asia yatakayofanyika nchini Indonesia mwezi Agosti mwaka 2018.