Valencia, Matic, Herrera na Sanchez warejea kikosini kupiga Spurs
Na Geoffrey Anene
Manchester United imepigwa jeki na kurejea kikosini kwa wachezaji nyota Antonio Valencia, Nemanja Matic, Ander Herrera na Alexis Sanchez kabla ya kumenyana na Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, Jumatatu (10.00pm).
Nyota hawa walikosa mechi ya Brighton & Hove, ambayo United ya kocha Jose Mourinho ililambishwa sakafu ugenini kwa mabao 3-2 Agosti 19.
Valencia, Matic na Herrera watakuwa wakionja mechi yao ya kwanza ligini msimu huu naye Sanchez anarejea baada ya kushiriki mchuano wa ufunguzi dhidi ya Leicester City, ambao United ilishinda 2-1 uwanjani Old Trafford. Alipata jeraha dhidi ya Leicester, lakini anaonekana yuko fiti kukabiliana na Spurs.
Mkenya Victor Wanyama pamoja na raia wa Korea Kusini Heung-min Son, na Mholanzi Vincent Janssen hawatawakilisha timu yao ya Spus katika mchuano huu. Wanyama na Janssen wanauguza majeraha naye Son anawakilisha taifa lake katika mashindano ya Bara Asia yanayoendelea nchini Indonesia.
Tangu mechi ya mkondo wa kwanza ya msimu 2015-2016, timu hizi zimekuwa zikishinda mechi ya nyumbani zinapokutana. Msimu uliopita, Spurs ilishinda 2-0 uwanjani Wembley kabla ya kusalimu amri 2-1 uwanjani Old Trafford. Zitakutana uwanjani Old Trafford leo. Mara ya mwisho Tottenham ilishinda uwanjani humu ilikuwa 2-1 Januari 1 mwaka 2014 kupitia Emmanuel Adebayor na Christian Eriksen. Danny Welbeck alifungia United bao la kufutia machozi.
Vikosi:
Manchester United
Makipa – David de Gea, Lee Grant;
Mabeki – Antonio Valencia, Matteo Darmian, Chris Smalling, Victor Lindelof, Phil Jones, Ashley Young, Luke Shaw;
Viungo – Nemanja Matic, Scott McTominay, Fred, Andreas Pereira, Jesse Lingard, Ander Herrera, Juan Mata, Paul Pogba, Marouane Fellaini;
Washambuliaji – Marcus Rashford, Romelu Lukaku, Alexis Sanchez
Tottenham
Lloris; Vertonghen, Alderweireld, Sanchez; Trippier, Davies, Dier, Eriksen, Alli, Lucas; Kane.