• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Van Dijk mbioni kushinda tuzo ya mwanasoka bora duniani

Van Dijk mbioni kushinda tuzo ya mwanasoka bora duniani

Na GEOFFREY ANENE

VIRGIL Van Dijk yumo mbioni kushinda tuzo ya mwanasoka bora duniani ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) baada ya kujumuishwa katika orodha ya wawaniaji 10 wa tuzo hiyo ya kifahari Jumatatu.

Beki huyu wa Uholanzi na klabu ya Liverpool nchini Uingereza, ambaye Agosti 29 alinyakua tuzo ya mwanasoka bora barani Ulaya (Uefa) wa mwaka 2018-2019, atawania tuzo hiyo dunia dhidi ya wachezaji wenza Sadio Mane na mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2017 na 2018 Mohamed Salah, ambao ni washambuliaji.

Wawaniaji wengine wa tuzo hiyo ya Fifa inayonuia kupongeza wachezaji waliong’ara kati ya Julai 16 mwaka 2018 na Julai 19 mwaka 2019 ni mvamizi matata wa Tottenham Hotspur na Uingereza Harry Kane na kiungo wa zamani wa Chelsea, Mbelgiji Eden Hazard, ambaye sasa yuko Real Madrid.

Wachezaji hawa watano wanaungana na masupasta Lionel Messi (Barcelona & Argentina) na Cristiano Ronaldo (Juventus na Ureno) na Mfaransa Kylian Mbappe anayesakata soka yake katika klabu ya Paris Saint-Germain.

Makinda Waholanzi Frenkie de Jong na Matthijs de Ligt, ambao walibeba Ajax Amsterdam kushinda Ligi Kuu ya Uholanzi na pia kufikisha klabu hiyo katika nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya, wanakamilisha orodha ya wawaniaji 10.

Orodha hii itakatwa hadi wawaniaji watatu katika wiki chache zijazo kabla ya mshindi kutawazwa mjini Milan nchini Italia mnamo Septemba 23, 2019.

Messi na Ronaldo walitawala tuzo hii kutoka mwaka 2008 kabla ya raia wa Croatia Luka Modric kuibuka mshindi mwaka 2018.

Mshambuliaji Messi alishinda mwaka 2009, 2010, 2011, 2012 na 2015 naye Ronaldo akatawala mwaka 2008, 2013, 2014, 2016 na 2017.

Mwanasoka bora nchini Uingereza

Van Dijk, ambaye alifagia tuzo ya mwanasoka bora nchini Uingereza msimu 2018-2019 pamoja na kuibuka mwanasoka bora wa klabu ya Liverpool, mashabiki wa Liverpool, wasakataji wa kabumbu nchini Uingereza na pia kuwa mwanasoka bora wa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Tottenham Hotspur mnamo Juni 1, 2019, anapigiwa upatu mkubwa sana wa kubeba taji la mwanasoka bora duniani mwaka 2019.

Atakuwa beki wa kwanza kutwaa tuzo hiyo tangu Mwitaliano Fabio Cannavaro mwaka 2006.

Aidha, mmoja kutoka orodha ya Jurgen Klopp (Liverpool), Pep Guardiola (Manchester City) na Mauricio Pochettino (Spurs) atatawazwa Kocha Bora wa mwaka 2019 katika hafla hiyo ambayo huwa na vitengo kadhaa kikiwemo mwanasoka bora mwanadada.

You can share this post!

SIHA NA ULIMBWENDE: Matumizi mbalimbali ya mshubiri

Klabu za EPL kupiga abautani kuhusu kufunga kipindi cha...

adminleo