Michezo

Vardy awabeba Leicester City hadi hatua ya 32-bora ya Europa League

November 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

JAMIE Vardy alifunga bao la dakika za majeruhi na kuwasaidia Leicester City kufuzu kwa hatua ya 32-bora ya Europa League baada ya kusajili sare ya 3-3 dhidi ya Braga ya Ureno mnamo Novemba 26, 2020.

Fowadi huyo raia wa Uingereza aliingia ugani katika kipindi cha pili na kujaza kimiani krosi safi aliyopokezwa na Marc Albrighton katika dakika ya 95.

Hiyo ilikuwa mechi ya tatu kwa Leicester kutoka nyuma na kulazimisha sare dhidi ya wapinzani.

Al Musrati aliwaweka Braga kifua mbele katika dakika ya nne kabla ya Harvey Barnes kusawazisha mambo dakika tano baadaye. Hata hivyo, Dias Fernandes Paulinho aliwafungia wenyeji Braga bao la pili katika dakika ya 24 kabla ya Luke Thomas kuzifuta juhudi zake.

Ingawa Rodrigues Barbosa Fransergio alicheka na nyavu za Leicester katika dakika ya 90, Vardy alihakikisha kwamba wanagawa alama katika mchuano huo alipopachika wavuni bao la tatu lililosawazisha mambo sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchuano kupulizwa.

Ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na Zorya Luhansk dhidi ya AEK Athens katika mchuano mwingine wa Kundi G uliwapa Leicester uhakika wa kusonga mbele chini ya mkufunzi Brendan Rodgers.

Leicester almaarufu ‘The Foxes’ walimtegemea sana kipa Kasper Schmeichel aliyefanya kazi ya ziada na kuwanyima wavamizi wa Braga nafasi nyingi za wazi. Leicester waliingia ugani wakijivunia ushindi wa 4-0 dhidi ya Braga katika gozi la awali, jambo ambalo lilimchochea Rodgers kupanga kikosi dhaifu dhidi ya wenyeji wao.

Hata hivyo, ujio wa Wesley Fofana, Youri Tielemans, Vardy na James Maddison ulibadilisha kasi ya mchezo na kuwatambisha Leicester mwishoni mwa kipindi cha pili.