Michezo

Victor Osimhen mwanasoka ghali zaidi Ulaya Mwafrika

August 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

NAPOLI wanaoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A) wamemsajili mshambuliaji chipukizi mzawa wa Nigeria, Victor Osimhen kutoka Lille ya Ufaransa.

Katika taarifa yao, Napoli walibana maelezo mengi muhimu kuhusiana na usajili wa fowadi huyu na badala yake kusema: “Tunafurahi sana kutangaza kwamba tumemsajili Osimhen kwa mkataba wa kudumu kutoka Lille.”

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe nchini Ufaransa, uhamisho wa Osimhen unakadiriwa kugharimu Napoli kima cha Sh9.6 bilioni, fedha zinazomfanya kuwa mwanasoka ghali zaidi kutoka barani Afrika.

Ina maana kwamba Napoli kwa sasa wameweka mezani kitita kinono zaidi kuliko kile ambacho Arsenal walitoa kwa minajili ya huduma za fowadi mzawa wa Ivory Coast, Nicolas Pepe aliyeagana na Lille mwaka mmoja uliopita.

Osimhen alijiunga na Lille mwanzoni mwa msimu huu wa 2019-20 kuwa kizibo kamili cha Pepe baada ya kushawishiwa na Lille kuagana na Charleroi inayonogesha Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Baada ya kufunga jumla ya mabao 18 katika mapambano yote ya msimu huu akivalia jezi za Lille, Osimhen mwenye umri wa miaka 21 alianza kuhusishwa na Napoli mapema sana katika mwezi wa Juni, 2020.

Ni katika mwezi huo ambapo alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kambini mwa Lille na pia akajumuishwa kwenye kikosi cha wanasoka bora 11 cha Ligue 1 msimu huu.

Osimhen alianza kupata umaarufu katika ulingo wa soka mnamo 2015 wakati wa fainali za Kombe la Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 nchini Chile. Aliibuka mfungaji bora na mwanasoka aliyechangia idadi kubwa zaidi ya magoli katika mapambano hayo yaliyoshuhudia wavulana wa Nigeria almaarufu ‘Golden Eaglets’ kutwaa ubingwa.

Akiwa na umri wa miaka 16 pekee wakati huo, Osimhen alipachika wavuni jumla ya mabao 10 baada ya kufunga kila mechi ambayo Nigeria walisakata. Ufanisi wake katika fainali hizo za Kombe la Dunia zilimfanya kutawazwa Chipukizi Bora wa Mwaka barani Afrika mnamo 2015.

Kudhihirika kwa ukubwa wa kipaji chake katika kipute hicho kulimtia kwenye rada ya klabu nyingi maarufu za bara Ulaya. Hata hivyo, alihiari kuyoyomea Ujerumani kuvalia jezi za VfL Wolfsburg ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Baada ya msimu wake kuvurugwa pakubwa na misururu ya majeraha mabaya, Osimhen ambaye hakufunga bao lolote katika jumla ya michuano 16 ndani ya jezi za Wolfsburg, alitafuta hifadhi mpya kambini mwa Charleroi waliowahi kujivunia huduma zake kwa mkopo kabla ya kumpokeza mkataba wa kudumu. Alifunga jumla ya magoli 19 katika msimu wake wa kwanza kambini mwa kikosi hicho cha Ubelgiji.