Michezo

Victor ‘Rabbit’ Chumo kumwekea kasi Kipchoge katika mbio za London Marathon

August 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa mbio za Barcelona Half Marathon, Victor ‘Rabbit’ Chumo, atakuwa miongoni mwa wanariadha watakaoweka kasi kwenye kivumbi cha London Marathon, Uingereza mnamo Oktoba 4.

Chumo atamtia kasi Eliud Kipchoge ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia kwenye mbio hizo za kilomita 42. Bingwa mara nne wa dunia na Olimpiki katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 Mo Farah, atawawekea kasi Waingereza Matt Clowes na Jake Smith wanaopania kutumia London Marathon kusajili muda wa kufuzu kwa Olimpiki za Tokyo, Japan mnamo 2021.

Akishiriki mbio za kilomita 42 kwa mara ya kwanza, Farah aliibuka mshindi wa Chicago Marathon kwa muda wa saa 2:05:11 mnamo 2018.

“Kivumbi cha London Marathon kitakuwa na upekee na msisimko mkubwa. Kitashirikisha wanariadha wa haiba ya juu na kibarua nilicho nacho mbele yangu si chepesi,” akasema Chumo.

Kipchoge anashikilia rekodi ya dunia ya marathon ya saa 2:01:39 aliyoweka mnamo 2018 alipotia kibindoni taji la Berlin Marathon nchini Ujerumani. Atakuwa akilenga kutetea ufalme wake jijini London.

“Nimepiga mazoezi kwa zaidi ya miezi minne sasa. Niko katika hali nzuri na fomu yangu inaridhisha. Kubwa katika matamanio yangu ni kutetea taji. Lakini iwapo muda uliosalia utanipa fursa ya kuboreka hata zaidi, basi ninaweza kuwazia uwezekano wa kuvunja rekodi yangu,” akasema Kipchoge

Kwa upande wake, Bekele ambaye ni mzawa wa Ethiopia, alikosa fursa ya kuifikia rekodi ya Kipchoge kwa sekunde mbili pekee mnamo Septemba 2019 baada ya kuibuka mshindi wa Berlin Marathon kwa muda wa saa 2:01:41.

Kipchoge na Bekele ndio wanaojivunia muda wa kasi ya juu zaidi katika historia ya mbio za kilomita 42 duniani.

“Nashiriki mazoezi kwa kukimbia umbali wa angalau kilomita 30 kila siku. Sasa napania kutumia muda uliosalia kabla ya kutua London kuimarisha kasi yangu,” akasema Chumo ambaye atakuwa akimwekea Kipchoge kasi katika mbio za marathon kwa mara ya tatu.

“Nilikuwa sehemu ya watimkaji waliomtia kasi Kipchoge katika Marathon ya Nike Breaking 2 aliyoishinda kwa muda wa saa 2:00:25 mnamo Mei 6, 2017, nchini Italia,” akaongeza.

Chumo alikuwa pia katika kundi la wanariadha waliomtia kasi Kipchoge wakati alipoweka historia ya kuwa mwanadamu wa kwanza kuwahi kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili.

Kipchoge alitumia saa 1:59:40 kukamilisha mbio hizo za Ineos 1:59 Challenge jijini Vienna, Austria mnamo Oktoba 2019.

“Tangu wakati huo, amekuwa na imani kubwa kwangu na itanilzimu kujitahidi kadri ya uwezo wangu kuhakikisha kwamba ndoto yake ya kushinda mbio za London Marathon inasalia hai,” akasema Chumo.

Kipchoge atakuwa akiwania fursa ya kutwaa ubingwa wa London Marathon mara tano baada ya kuibuka mshindi wa mbio hizo mnamo 2015, 2016, 2018 na 2019.

“Mbio za London Marathon zitakuwa kivutio kikubwa. Zitatoa jukwaa kwa wafalme wa riadha duniani kutifuana kivumbi na kuonyeshana ubabe. Jichoree picha hiyo akilini na uwaone Kipchoge, Bekele na Farah kwa mara ya kwanza wakitoana jasho ulingoni,” akaeleza Chumo ambaye ni mwanariadha wa zamani wa KDF.

Kipchoge na Bekele watalazimika pia kukabiliana na wapinzani tisa ambao wamewahi kukamilisha mbio za marathon kwa muda wa chini ya saa 2:06.

Hawa ni pamoja na Mosinet Geremew (2:02:55), Mule Wasihun (2:03:16), Sisay Lemma (2:03:36), Tamirat Tola (2:04:06), Marius Kipserem (2:04:11), Shura Kitata (2:04:49), Vincent Kipchumba (2:05:09), Sondre Nordstad Moen (2:05:48) na Gideon Kipketer (2:05:51).

Mbali na Chumo na Farah, wanariadha wengine watakaokuwa wakiweka kasi kwenye mbio hizo za London Marathon ni Erick Kiptanui, Alfred Barkach, Shadrack Kimining na Noah Kipkemoi aliyeshiriki Ineos 1:59 Challenge.