Michezo

Victor Wanyama apata jeraha la goti

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

NAHODHA wa Harambee Stars, Victor Wanyama amepata pigo kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza ya mwaka 2019-2020 kuanza baada ya kuumia goti.

Tovuti ya Spurs imesema kuwa kiungo huyu mkabaji aliripoti kuhisi usumbufu kwenye goti lake katika kipindi cha mazoezi cha Julai 29.

Kutokana na hali hiyo, waajiri wake Spurs waliamua kumuacha jijini London walipotaja kikosi cha kushiriki mashindano ya kujiandalia msimu mpya ya Audi Cup nchini Ujerumani.

Spurs ilichapa miamba wa Uhispania Real Madrid 1-0 katika mechi yake ya ufunguzi ya mashindano haya ya muondoano kupitia bao la Harry Kane hapo Julai 30 katika uwanja wa nyumbani wa Bayern Munich, Allianza Arena.

Itavaana na Bayern katika fainali mnamo Julai 31. Bayern ililipua miamba wa Uturuki, Fenerbahce 6-1 katika mechi nyingine Julai 30. Madrid na Fenerbahce zitalimana katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu Julai 31.

Wanyama amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha, hasa ya magoti kwa misimu miwili iliyopita. Yamempunguzia dakika uwanjani na kufanya Spurs kuwa tayari kumuuza kwa klabu yoyote itakayoweka mezani Sh1.1 bilioni.

Afanyiwa uchunguzi

Spurs sasa imesema kuwa ilimuacha London ili afanyiwe uchunguzi wa kimatibabu kwenye goti lake. Jeraha hilo linakuja wakati mbaya kwa sababu hajashiriki maandalizi ya msimu mpya kutokana na kuwa aliwakilisha Kenya katika Kombe la Afrika (AFCON) lililoanza Juni 21 na kutamatika Julai 19 nchini Misri.

Wanyama, ambaye alicheza mechi zote tatu za makundi za Kenya dhidi ya Algeria, Tanzania na Senegal, amekuwa likizoni.

Alihitaji zaidi kuwa na maandalizi mazuri ya msimu mpya, hasa wakati huu anakabiliwa na ushindani mkali katika safu ya kati baada ya Mfaransa Tanguy Ndombele kununuliwa kutoka Lyon nchini Ufaransa.