Vidal aingia rasmi kikosini Inter Milan
Na MASHIRIKA
INTER Milan wamekamilisha usajili wa kiungo mkabaji raia wa Chile, Arturo Vidal kutoka Barcelona kwa kima cha Sh126 milioni.
Vidal, 33, alifanyiwa vipimo vya afya jijini Milan, Italia mnamo Septemba 22 na uhamisho wake utakamilishwa chini ya kipindi cha saa 48 baadaye.
Kujiunga kwake na Inter kunamuunganisha tena na kocha Antonio Conte aliyewahi kumtia makali katika kikosi cha Juventus ambacho alikishindia jumla ya mataji matatu ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) katika kipindi cha misimu minne.
Inter wanatazamiwa kuanza kampeni za Serie A msimu huu dhidi ya Fiorentina mnamo Septemba 26, 2020 katika uwanja wao wa nyumbani wa San Siro.
Baada ya kuagana na wanasoka Arthur Melo aliyetua Juventus, Ivan Rakitic aliyejiunga na Sevilla na Nelson Semedo aliyeyoyomea Volves, Barcelona wanatarajiwa kukatiza uhusiano na idadi kubwa ya wachezaji chini ya kocha Ronald Koeman anayekisuka upya kikosi cha miamba hao wa soka ya Uhispania.
Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, ni wachezaji Marc-Andre ter Stegen, Gerard Pique, Frenkie de Jong, Antoine Griezmann, Lionel Messi na chipukizi Ansu Fati pekee ambao wana uhakika wa kusalia kambini mwa Barcelona.
Wachezaji wengine ambao wanatarajiwa kuagana rasmi na Barcelona muhula huu ni Jean-Clair Todibo, Rafinha, Nelson Semedo, Junior Firpo, Todibo, Samuel Umtiti, Ousmane Dembele na Luis Suarez.
Ingawa Suarez alihusishwa pakubwa na uwezekano wa kusajiliwa na Juventus, fowadi huyo wa zamani wa Liverpool amehiari kutua Atletico Madrid ya kocha Diego Simeone baada ya juhudi za kupata pasipoti na kibali cha kufanyia kazi Italia kugonga ukuta.
TAFSIRI: CHRIS ADUNGO