VIDUME KAMILI: Vidume vyapiga hatua AFCON, wanyonge nje
Na MASHIRIKA
CAIRO, Misri
BAADA ya kuongoza Kundi A kwa jumla ya pointi tisa na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya michuano ya AFCON, wenyeji Misri wakiongozwa na staa Mohamed Salah watakutana na Afrika Kusini, Jumamosi mbele ya mashabiki 75,000 katika mechi itakayochezewa uwanjani Cairo International.
Mapema, Morocco watakabiliana na Benin kwenye mechi nyingine ya hatua hiyo hapo kesho Ijumaa, huku Algeria wakivaana na Guinea hapo Jumapili, pia jijini hapa.
Limbukeni Madagascar watabakia mjini Alexandria, kupepetana na DR Congo katika uwanja ambao walishangaza kwa kuichapa Nigeria katika pambano la Kundi B.
Senegal ya kijana mwenye makali Sadio Mane imepangiwa kucheza na Uganda Cranes baada ya kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Harambee Stars ya Kenya katika mechi ya mwisho ya Kundi C, Jumatatu.
Mjini Ismailia, Mali ilifanya mabadiliko manane katika kikosi kilichocheza na Tunisia huku nahodha Abdoulay Diaby na mshambuliaji Moussa Marega wakiwa miongoni mwa waliokuwa katika kikosi cha akiba katika kabiliano la Jumanne.
Aidha kocha kocha Aliou Cisse wa Senegal amewaonya wachezaji wake dhidi ya Uganda Cranes baada ya timu hizo kumaliza katika nafasi za pili katika makundi yao. Zinakutana katika 16-bora.
“Haitakuwa kazi rahisi mbele ya Uganda baada ya kushuhudia mechi zao za makundi,” Cisse aliwaambia waandishi baada ya kikosi chake kulaza Harambee Stars mabao 3-0 katika mechi ya mwisho ya Kundi C, Jumatatu.
“Lazima tujipange vyema dhidi ya Uganda kwa sababu wamethibitisha uwezo wao tangu michuano hii ianze,” aliongeza kocha huyo.
“Sote tumefuzu moja kwa moja bila kutegemea mahesabu, na sasa itakuwa vigumu zaidi kwa sababu wameshindwa mechi chache siku za karibuni,” alisema.
Senegal na Uganda zilikutana kwa mara ya mwisho wakati wa mechi za mchujo wa Kombe la Dunia la 2014 ambapo Senegal iliibuka na ushindi wa 1-0, bao lililofungwa na Sadio Mane mechi ikielekea kumalizika.
Kwa upande mwingine, Abdu Lumala wa Uganda Cranes naye amewahimiza wenzake waendelee kujinoa kwa pambano hilo linalotazamiwa kuwa gumu. Mshambuliaji huyo ameibukia kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia maskauti waliofika hapa kutafuta wachezaji wapya kujiunga na klabu zao za ligi kubwa barani Ulaya.
Nyota huyo wa klabu ya Syrianska ya Uswidi anaamini wanaweza kupata matokeo mazuri dhidi ya Senegal iwapo watacheza kwa ushirikano.
“Kujitolea kwa kila mchezaji katika mechi hii kutakuwa na faida kubwa kwa kikosi kizima,” alisema nyota huyo mwenye umri wa miaka 21.
“Nawapongeza wenzangu kwa kunisaidia kuimarisha kiwango changu, kiasi cha kuanza kuvutia klabu nyingi ambazo zimeanza kuonyesha nia ya kunisajili,” aliongeza.
“Nawaomba mashabiki wetu wazidi kutuunga mkono hadi dakika ya mwisho,” alisema nyota huyo.
Matumini ya Harambee Stars kufuzu kwa hatua hiyo yalivurugwa baada ya Benin kuagana bila kufungana na Cameroon katika pambano la Kundi E. Nayo Mali iliyotegemewa na Wakenya kuisaidia kufuzu ilifanya kweli kwa kushinda Angola, katika kundi hilo la E. Kenya ilihitaji msaada wa Benin na Angola kwa wakati mmoja.
Kuondoka kwa Harambee Stars mapema kumewashangaza wengi baada ya Madagascar ambao walipokea kichapo cha 1-0 kutoka kwa timu hiyo ya Kenya kwenye mechi ya kupimana nguvu nchini Ufaransa kufuzu kwa hatua ya 16-bora hasa baada ya kutandika miamba Super Eagles (Nigeria).
Algeria ambao wamepangiwa kucheza na Guinea wameonyesha dalili ya kutwaa ubingwa wa mwaka huu ikizingatiwa jinsi walivyomaliza mechi zao bila kushindwa, wala kutoka sare.
Ratiba ya mechi za raundi ya 16-bora ni:
Ijumaa – Morocco na Benin (Al Salam Stadium, saa kumi na mbili jioni),
Uganda na Senegal (Cairo Stadium, saa tatu usiku, Jumamosi)
Jumamosi- Nigeria na Cameroon (Alexandria Stadium, Jumamosi, saa kumi na mbili);
Misri na Afrika Kusini (Cairo Stadium, saa tatu, Jumapili); Jumapili- Madagascar na DR Congo (Alexandria Stadium, saa kumi na mbili), Algeria na Guinea (June 30 Stadium, saa tatu usiku, Jumatatu); Jumatatu – Mali na Cote d’Ivoire (Suez Stadium, saa kumi na mbili), Ghana na Tunisia (Ismailia Stadium, saa tatu, Jumanne).