Michezo

Vihiga United waingiwa na hofu wanapojiandaa kwa mchujo

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

 

CHRIS ADUNGO

KOCHA Sammy Okoth wa Vihiga United ni mwingi wa hofu kadri anavyokiandaa kikosi chake kuvaana na Kisumu All Stars katika mchujo wa Ligi Kuu ya Kenya na Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Vikosi hivyo vitavaana kwenye mechi za mikondo miwili ya kubaini klabu ya ziada itakayoshuka daraja kwenye Ligi Kuu ya FKFPL msimu ujao na kitakachopanda ngazi kutoka NSL kwa minajili ya kinyang’anyiro cha muhula mpya wa 2020-21.

Mechi ya mkondo wa kwanza itasakatwa mnamo Oktoba 7 na marudiano kuandaliwa Oktoba 11. Maamuzi ya nani atakayekuwa mwenyeji wa mkondo wa kwanza wa mchujo huo yatafanywa leo kwa mujibu wa kifungu cha 2.9.2 cha Sheria za FKF na Ligi Kuu ya soka ya humu nchini.

Kisumu All-Stars walishikilia nafasi ya 16 kwenye jedwali la vikosi 18 vya KPL mnamo 2019-20 huku Vihiga United wakimaliza kampeni za NSL katika nafasi ya tatu nyuma ya Bidco United na Nairobi City Stars waliokwezwa daraja kunogesha Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa mujibu wa Okoth, wengi wa wanasoka wake waliorejea kambini mnamo Jumatano wiki hii hawako katika fomu ya kuridhisha na wameongeza uzani baada ya kutoshiriki mechi yoyote kwa zaidi ya miezi mitano iliyopita.

Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa Zoo FC amesema kwamba kikosi chake kitalazimika kushiriki mazoezi makali zaidi katika kipindi cha wiki mbili zijazo kabla ya kuwapa wanasoka wake mikakati kabambe itakayowasaidia kuwadengua All Stars.

“Nilianza kupokea wachezaji mnamo Jumatano. Nilibaini kuwa wengi wao wamenenepa zaidi na hili ni jambo linalonikosesha usingizi,” akasema mwanasoka huyo wa zamani wa Harambee Stars.

Licha ya panda-shuka tele zinazokabili wapinzani wao, Okoth amewataka wanasoka wake kutowabeza All Stars ambao kwa pamoja na Western Stima, wana kiu ya kuendelea kuwakilisha eneo la Nyanza katika soka ya Ligi Kuu ya Kenya muhula ujao.

“All Stars wana hamu ya kusalia ligini na watapania kufanya chochote kilicho ndani ya uwezo wao ili kuweka hai maazimio hayo. Mbali na kujivunia idadi kubwa ya mashabiki, pia wana wachezaji wazuri wenye uzoefu mpana na tajriba pevu,” akaongeza.

Kwa upande wao, Nicholas Ochieng ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa All Stars amesema kwamba Andrew Oroka atasimamia michuano miwili ijayo dhidi ya Vihiga United.

Kikosi hicho kilitangaza nafasi za kazi katika benchi nzima ya kiufundi mwezi uliopita.

“Bado hatujapata kocha mpya lakini Aroka tutamtegemea Aroka kutuongoza katika mechi mbili zijazo. Amekuwa na kikosi kwa muda mrefu na miongoni mwa wakufunzi ambao wametuma maombi ya kupokezwa kazi ya ukocha,” akasema Ochieng kwa kufichua kwamba wanapania pia kuajiri mkufunzi msaidizi, kocha wa viungo vya mwili na mkufunzi wa makipa.

Hii ni baada ya All Stars kuagana rasmi na Jeff Odongo (kocha wa viungo vya mwili) na Fredrick Onyango (kocha wa makipa) walioteuliwa kuhudumu katika benchi ya kiufundi mnamo Februari 2020.

Aroka ndiye afisa aliyewahi kuhudumu kambini mwa kikosi hicho kinachodhaminiwa na Serikali ya Kaunti ya Kisumu kwa muda mrefu zaidi na ndiye aliyechangia kupandishwa ngazi kwa kikosi hicho kushiriki soka ya Ligi Kuu mwanzoni mwa msimu huu wa 2019-20.

Mnamo Januari 2020, All Stars walimtimua aliyekuwa kocha wao wa muda mrefu, marehemu Henry Omino kwa pamoja na aliyekuwa msaidizi wake, Aroka na kocha wa makipa Joseph Ongoro kwa sababu ya matokeo duni ya kikosi.

Hata hivyo, Aroka alirejea baadaye kambini mwa klabu hiyo baada ya Arthur Opiyo aliyeteuliwa kushikilia mikoba ya kikosi hicho kwa muda kurejea Ujerumani kwa mafunzo zaidi ya ukocha.

Mbali na Aroka, wengine ambao wametuma upya maombi ya kazi kambini mwa All Stars ni Odongo na Onyango.

“Walikuwa wametia saini mikataba ya miezi michache ambayo kwa sasa imekatika. Wamewasilisha upya maombi ya kazi kwa minajili ya kuendelea kuhudumu nasi katika benchi mpya ya kiufundi ambayo tunapania kuifichua rasmi mwishoni mwa Septemba,” akasema Ochieng kwa kusisitiza kwamba wanamtafuta kocha mkuu aliye na leseni ya kiwango cha C kutoka kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).