Michezo

Vijana wa Kimanzi watua Uzbekistan, mechi zasongeshwa

March 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MECHI za kirafiki kati ya Emerging Stars ya Kenya na mabingwa wa Bara Asia, Uzbekistan zimesukumwa mbele siku moja kutoka Machi 22 na Machi 25 hadi Machi 23 na Machi 26.

Stars ya kocha Francis Kimanzi, ambayo ilipaa kwa ndege katika uwanja wa kimataifa ya Jomo Kenyatta jijini Nairobi Jumanne asubuhi, imefika salama salmini jijini Tashkent Jumatano asubuhi.

Taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Uzbekistan (UFF) zimesema Jumatano kwamba mechi ya kwanza itapigiwa uwanjani Barkamol Avlod mjini Andijan, huku ya pili ikiandaliwa katika uwanja wa Istiqol mjini Fergana. Mechi zote zitasakatwa saa kumi na mbili jioni saa za Kenya (saa mbili usiku saa za Uzbekistan).

Kikosi cha Emerging Stars chakaribishwa Uzbekistan. Picha/ Hisani

Timu zote mbili zinatumia michuano hii kujiweka tayari kwa mechi za kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo nchini Japan mwaka 2020.

Uzbekistan haijawahi kuwakilishwa katika soka kwenye Olimpiki licha ya kujaribu kufuzu kwa makala ya mwaka 2004, 2008, 2012 na 2016.

Hata hivyo, Uzbekistan si timu rahisi. Ilipiga kila timu isipokuwa Qatar katika mashindano ya Bara Asia mwezi Januari mwaka 2018 na kutawazwa mabingwa.

Katika kombe hilo lililofanyika nchini Qatar, Uzbekistan ililemewa 1-0 na Qatar katika mechi ya ufunguzi kabla ya kulima Uchina na Oman 1-0 kila mmoja na kuingia robo-fainali. Ilicharaza Japan 4-0 katika robo-fainali kabla ya kunyamazisha Korea Kusini 4-1 katika nusu-fainali. Uzbekistan ilinyakua taji baada ya kuzima Vietnam 2-1 katika muda wa ziada kwenye fainali Januari 27, 2018.

Kwa upande wake, timu ya Kenya pia haijawahi kushiriki Olimpiki. Itaingia mchuano huu bila uzoefu wowote wa kimataifa. Haijapiga mechi yoyote ya kimataifa. Hata hivyo, kikosi cha Kimanzi kinajumuisha wachezaji kadhaa walio na ujuzi kwenye Ligi Kuu kama Teddy Osok (Sofapaka), Cliff Kasuti (Ulinzi Stars) na Nicholas Kipkirui (Zoo Kericho).

Kocha Kimanzi akihojiwa na wanahabari wa Uzbekistan. Picha/ Hisani

Kikosi cha Kenya:

Makipa

Timothy Odhiambo (Ulinzi Stars), Job Ochieng (Mathare United)

Mabeki

Mike Kibwage (AFC Leopards), Joseph Okumu (hana klabu), Benard Ochieng (Vihiga United), Bolton Omwenga (Kariobangi Sharks), David Owino (Mathare United)

Viungo

Teddy Osok (Sofapaka), Sven Yidah (Kariobangi Sharks), Siraj Mohammed (Bandari), Chrispinus Onyango (KCB), Abdalla Ahmed (Mathare United), Ibrahim Shambi (Ulinzi Stars), James Mazembe (Kariobangi Sharks), Henry Juma (Kariobangi Sharks), Cliff Kasuti (Ulinzi Stars)

Washambuliaji

Pistone Mutamba (Wazito), Amai Atariza (Bandari), Jafari Owiti (AFC Leopards), Brian Yator (KCB), Nicholas Kipkirui (Zoo Kericho), Daniel Okoth Otieno (Sony Sugar).