Michezo

VIKEMBE: Mtoto Anzu Fati hakamatiki yule!

March 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na GEOFFREY ANENE

ANSSUMANE ‘Ansu’ Fati Vieira ni mchezaji wa soka aliyejaliwa kipawa adimu cha winga wa pembeni kushoto anayechezea mabingwa Barcelona nchini Uhispania.

Kinda huyu matata, ambaye husherehekea siku yake ya kuzaliwa Oktoba 31 sawa na gunge Zlatan Ibrahimovic, ametoka mbali kufikia kiwango cha kuaminika na yu mbioni kuwa Lionel Messi mpya.

Messi, 32 aliye raia wa Argentina, amekuwa akifanyia Barcelona makubwa uwanjani tangu 2004, lakini atakuwa akiangika daluga zake miaka michache ijayo.

Ansu alizaliwa miaka 17 iliyopita mjini Bissau nchini Guinea-Bissau wakati mwanasoka bora duniani Messi alipokuwa anakaribia kumaliza miaka miwili katika akademia ya soka ya Barcelona almaarufu La Masia.

Babaye Bori Fati alikuwa dereva na mamaye Lurdes yaya mjini Bissau.

Umaskini pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe na mapinduzi nchini Guinea-Bissau vilisukuma Bori kuondoka Guinea-Bissau kutafutia familia yake maisha mazuri nchini Ureno.

Mambo hayakuwa mazuri Ureno lakini akapata mpenyo nchini Uhispania. Hata hivyo, maisha yalikuwa magumu kwa babaye Ansu, hali iliyomlazimu kuwa ombaomba kabla ya kupata kazi ya kuwa dereva wa meya wa mji wa Seville na kufanikiwa kuleta familia yake mjini humo kupitia usaidizi wa meya huyo.

Wakati familia hiyo ilitua Seville, Ansu alikuwa na umri wa miaka sita.

Hapa ndipo soka ya Ansu ilianzia. Alikuwa shabiki wa mahasimu wakuu wa Barcelona, Real Madrid.

Alienzi sana supastaa Cristiano Ronaldo aliyekuwa akichezea Madrid.

Alipokuwa akijifunza soka, kakaye Braima alifanyiwa majaribio na klabu ya Sevilla na kupita. Hatua ya Braima kujiunga na Sevilla ilipatia Ansu ari ya kuwa msakataji wa kabumbu.

Ansu alihudhuria majaribio katika klabu ya Sevilla na nyingine zilizopatikana karibu na maeneo hayo.

Ingawa hakufaulu kujiunga na Sevilla, Ansu alinyakuliwa na klabu ya Herrera inayopatikana katika mkoa huo wa Seville.

Alikuwa Herrera msimu mmoja kabla ya Sevilla kumkubali katika akademia yake ilipoona talanta yake ilivyozivutia Real Madrid na Barcelona.

Mavizio ya miamba hao wa soka ya Uhispania yaliletea Ansu karaha. Sevilla ilipopokea habari kuwa maskauti wa Madrid na Barcelona walifika nyumbani kwao kujaribu kushawishi wazazi wake wamruhusu ajiunge na mmoja wao, haikuchezesha Ansu kwa mwaka mzima.

Ansu hakufa moyo. Ndoto yake ya kuwa mwanasoka ilifufuliwa na akademia ya Barcelona iliyoamua kumchukua akiwa na umri wa miaka tisa na kuanzisha tena uchezaji wake wa soka. Hakuwa amepiga kutu.

Aliridhisha haraka katika akademia hiyo. Talanta yake na sifa zake za kuongoza timu hiyo zilishuhudia wakati mmoja akitwikwa majukumu ya nahodha. Hata hivyo, ukuaji wake ulipata pigo Desemba 2015.

Alivyogwa mguu wake wa kulia na mchezaji wa Espanyol na kuvunjika. Kwa miezi 10, Ansu alikuwa akitibiwa jeraha hilo. Kipindi hicho kilitarajiwa kuwa kitamfifisha moyo, lakini kilimfanya apate nguvu ya kuthibitishia ulimwengu bado ana tamaa ya kutimiza ndoto ya kuwa mwanasoka wa kulipwa.

Baada ya kupona na kurejea ulingoni, Ansu aliimarika katika miezi iliyofuata na kufikia kiwango cha kuwa mchezaji aliyevutia zaidi katika akademia ya klabu hiyo.

Alitawala soka ya chipukizi na haikumchukua muda kabla ya kupata kandarasi yake ya kwanza ya kutandaza soka ya kulipwa mnamo Julai 24, 2019.

Ansu alipewa fursa ya kuonyesha talanta yake katika timu ya watu wazima alipokuwa na umri wa miaka 16 na siku 298. Kocha Ernesto Velverde aliamua kumtumia kama mchezaji wa akiba kwa mara ya kwanza ligini mnamo Agosti 25, 2019 washambuliaji Ousmane Dembele, Messi na Luis Suarez wakiwa nje wakiuguza majeraha.

Tangu wakati huo, Ansu ameng’ara akivalia jezi ya Barca ligini, Klabu Bingwa Ulaya na Copa del Rey na kupata kibali cha kupeperusha bendera ya Uhipania kimataifa kutoka kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) baada ya kupata uraia wa taifa hilo Septemba 2019.

Ansu, ambaye utajiri wake tayari unazidi Sh400 milioni, alisaini kandarasi mpya Desemba 2019 hadi mwaka 2022 inayomruhusu kutoka uwanjani Camp Nou kwa Sh18.9 bilioni.

Kinachofanya Ansu aaminike atakuwa kizibo tosha cha Messi ni kuwa supastaa Messi alihitaji mechi 13 kupata magoli yake mawili ya kwanza. Ansu alipata idadi hiyo ya mabao katika mechi tatu