Vikosi 8 kushiriki fainali za Chapa Dimba wikendi
Na CECIL ODONGO
TIMU nane zinatarajiwa kupigania ubabe kwenye mchezo wa soka wikendi hii ili kutwaa taji la ubingwa wa mashindano ya Chapa Dimba na Safaricom eneo la Nairobi.
Makala ya mashindano hayo ukanda wa Nairobi yataandaliwa Jumamosi na Jumapili katika uwanja wa Shule ya Upili ya Jamhuri jijini Nairobi.
Kwenye kitengo cha wavulana, washindi wa makala ya mwaka 2019 South B United kutoka Starehe walikosa kutinga hatua ya makundi na sasa ni wazi kwamba bingwa mpya atatangazwa jijini Jumapili.
Hata hivyo, akina dada wa Acakoro kutoka Kasarani ambao walishinda ubingwa wa mwaka 2019 watakuwa ange kutetea taji lao.
Mshirikishi wa Chapa Dimba na Safaricom ukanda wa Nairobi James Omondi, alisema timu nyingi zilisajiliwa mwaka huu na kufanya mashindano hayo kuwa na ushindani mkali mno.
“Timu nyingi zilisajiliwa eneo la Nairobi kuliko mwaka jana na kufanya makala ya mwaka huu kuwa na ushindani mkali hata kabla kipute chenyewe kung’oa nanga. Ningependa kuwarai wachezaji wawe na nidhamu ili wasiondolewe mashindanoni,” akasema Omondi.
Timu ambazo zitatifua vumbi upande wa wavulana ni Kenya School of Government (KSG) kutoka Westlands, Shule ya mseto ya Dagoretti, Hakati Sportiff ya Makadara na Brookshine Academy kutoka Kasarani.
Upande wa wanadada, mabingwa watetezi Acakoro watapigania kuhifadhi taji lao kwa kutoana kijasho na St Anne’s Eaglets ya Makadara, Kibagare ya Westlands na Beijing Raiders kutoka Starehe.
Timu 100 zilishiriki mechi za kufuzu eneo la Nairobi, lakini timu hizo nane pekee ndizo zilitwaa ushindi na kufuzu mashindano hayo ya kieneo.
Washindi wa mechi za wikendi upande wa wavulana na wasichana watatuzwa Sh200,000 kila mmoja. Pia watapata nafasi ya kuwakilisha Nairobi kwenye fainali ya kitaifa itakayoandaliwa Juni, 2020.
Timu zitakazomaliza katika nafasi ya pili nazo zitapokezwa Sh100,000 huku wachezaji waliong’aa pia wakijizolea tuzo mbalimbali.
Tayari Pwani, Mashariki, Kati na Kaskazini Mashariki wametoa timu za kushiriki fainali hiyo ya kitaifa. Shule ya Tumaini na ile ya wasichana ya Isiolo zitawakilisha ukanda wa Mashariki huku Yanga SC ya Malindi na wanadada wa Kwale zikiwakilisha Pwani.
Eneo la Kati litawakilishwa na Falling Waters ya Laikipia na Ulinzi Youth kutoka Nanyuki. Berlin FC kutoka Garissa ndiyo watashiriki fainali kutoka ukanda wa Kaskazini Mashariki.
Mshindi wa makala ya kitaifa, atatuzwa donge nono ya Sh1 milioni.