Michezo

Vikosi vitakavyowakilisha Kenya kwenye mashindano ya kimataifa msimu wa 2020-21 vikubaliwe kuanza mazoezi kikamilifu – kocha

October 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa timu ya taifa ya hoki ya wanawake, Jacqueline Mwangi, ameitaka serikali ikubalie vikosi vinavyojiandaa kwa vipute vya kimataifa kurejelea mazoezi ya kawaida.

Kenya inatazamiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya hoki katika eneo la Afrika Mashariki katika jitihada za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika zitakazofanyika kati ya Januari 18-24, 2021.

Bendera ya Kenya itapeperushwa na wanawake na wanaume kwenye mapambano hayo yaliyoahirishwa na kuratibiwa upya mnamo Mei 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Kikosi cha wanawake nchini Kenya kimetiwa kwenye zizi moja na Misri, Burundi, Libya, Ushelisheli, Sudan, Tanzania na Uganda. Mshindi wa kundi hilo atajikatia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Afrika zitakazoandaliwa Oktoba 2021.

Kwa mujibu wa Mwangi ambaye ni mchezaji wa zamani wa kimataifa, muda unazidi kuyoyoma na itakuwa vyema iwapo Kenya itaanza kujiandaa mapema kunoa vikosi pamoja na kuweka sawa mikakati itakayofanikisha maandalizi ya mapambano hayo.

“Kikosi kinahitaji kujiandaa vilivyo ndipo kisajili matokeo ya kuridhisha kwenye mapambano ya kimataifa. Itakuwa vyema iwapo serikali itakubalia wachezaji wa timu zitakazowakilisha Kenya kimataifa msimu huu wa 2020-21 kurejea uwanjani na kuanza mazoezi ili waoanishe mitindo ya kucheza kwao na kusuka njama za kuangusha wapinzani,” akasema Mwangi.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Hoki la Kenya (KHU), Wycliffe Ongori, amesema wanawasiliana na maafisa wa Wizara ya Michezo na dalili zote zinaashiria kwamba maombi yao yataidhinishwa punde.

Baadhi ya klabu za Ligi Kuu ya Soka ya Kenya, zikiwemo Gor Mahia na Kariobangi Sharks zimeanza kujiandaa kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21 huku wanariadha nao wakianza kujifua kwa michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan. Gor Mahia ambao ni mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya KPL, watawakilisha Kenya kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League).