Michezo

Villa wamsajili Martinez kutoka Arsenal

September 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

ASTON Villa wamemsajili kipa Emiliano Martinez kutoka Arsenal. Mkataba wake wa miaka minne umeramishwa kwa Sh2.4 bilioni.

Mlinda-lango huyo mwenye umri wa miaka 28 aliwajibishwa na Arsenal katika jumla ya mechi 23 msimu uliopita na akawa tegemeo kubwa katika fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea na mchuano wa Community Shield dhidi ya Liverpool.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal waliibuka washindi wa mechi hizo mbili zilizosakatiwa ugani Wembley, Uingereza.

Kocha Dean Smith wa Villa amesema kwamba Martinez atakuwa “nguzo muhimu katika kikosi chao kwa kipindi mrefu”.

“Ni nadra sana kupata fursa ya kumsajili kipa matata wa kiwango cha Martinez katika soka ya sasa kwa bei hiyo,” akaongeza Smith.

“Tunajua jinsi Arsenal walivyomstahi sana na tulishuhudia jinsi alivyoishia kuwa tegemeo kubwa kambini mwa kikosi hicho mwishoni mwa muhula uliopita kiasi cha kuwashindia mataji mawili muhimu,” akaeleza mkufunzi huyo.

Martinez anaondoka Arsenal baada ya kuhudumu uwanjani Emirates kwa miaka 10. Alijiunga na kikosi hicho akiwa chipukizi wa miaka 18 mnamo 2010.

Kuondoka kwake kulichochewa na maamuzi ya Arteta kumrejesha Bernd Leno kuwa kipa chaguo la kwanza la Arsenal baada ya Martinez kufichua kwamba ndiye aliyestahili sasa kuwajibishwa zaidi katika kikosi cha kwanza kuanzia muhula huu.

Leno alikuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal kilichowatandika Fulham 3-0 katika siku ya kwanza ya msimu huu wa 2020-21.

Martinez anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Villa muhula huu baada ya Ollie Watkins na Matty Cash waliotokea Brentford na Nottingham Forest mtawalia.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO