• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Vipimo vyabainisha wanasoka wawili kambini mwa Atletico Madrid wanaugua Covid-19

Vipimo vyabainisha wanasoka wawili kambini mwa Atletico Madrid wanaugua Covid-19

Na CHRIS ADUNGO

ATLETICO Madrid wamethibitisha kwamba wanasoka wawili katika kikosi chao kinachojiandaa kwa mechi ya robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) wamepatikana na virusi vya corona.

Miamba hao wa soka ya Uhispania (La Liga) wamesema Angel Correa, 25, na Sime Vrsaljko, 28, sasa wameshauriwa kurejea nyumbani na kujitenga.

Chini ya kocha Diego Simeone, Atletico wanatazamiwa kushuka dimbani kuvaana na RB Leipzig ya Ujerumani katika hatua ya nane-bora ya UEFA mnamo Alhamisi ya Agosti 13, 2020 jijini Lisbon, Ureno.

Ugonjwa wa Covid-19 ulifichuka kambini mwa Atletico baada ya wanasoka wote wa kikosi cha kwanza na maafisa wa klabu wanaojiandaa kufunga safari ya kuelekea Ujerumani kufanyiwa vipimo vya afya jijini Madrid, Uhispania.

Kwa sasa watapimwa tena hii leo Agosti 11 kwa pamoja na watu wote waliotangamana nao kwa karibu wakiwa katika uwanja wao wa Wanda Metropolitano.

“Tukio hili linatuweka katika ulazima wa kubadilisha ratiba yetu ya mazoezi na mfumo wa usafiri wa kuelekea Ureno pamoja na mipangilio yote ya malazi jijini Lisbon,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na vinara wa Atletico.

“Klabu itashirikiana sasa na vinara wa Uefa pamoja na maafisa husika wa afya ili kufanikisha ziara yetu na mapokezi jijini Lisbon,” ikaongeza taarifa hiyo kwa kusisitiza haja ya kudumishwa kwa heshima kwa wawili waliougua Covid-19 kambini mwao.

Kwa sababu ya janga la corona, kipute cha UEFA kinatazamiwa sasa kukamilishwa jijini Lisbon, Ureno ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki.

Mechi zote za robo-fainali na nusu-fainali zitakuwa za mkondo mmoja pekee na zitasakatwa kati ya Agosti 15-19. Fainali itatandaziwa jijini Lisbon, Ureno mnamo Agosti 23, siku mbili baada ya fainali ya Europa League kusakatiwa nchini Ujerumani.

You can share this post!

Phil Jones kukosa kampeni zilizosalia za Manchester United...

TANZIA: Mchezaji Ian Waraba wa Kenya Harlequins afariki...

adminleo