Michezo

Vipimo vyaonyesha Chris Froome hajapatikana na coronavirus

February 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MZAWA wa Kenya, Chris Froome hajapatikana na homa ya Coronavirus baada ya kupimwa kwenye mbio za kimataifa za baiskeli za UAE Tour zilizoshuhudia mikondo miwili ya mwisho ikifutiliwa mbali kwa hofu ya virusi hivyo hatari.

Taarifa kutoka nchi ya Milki za Kiarabu zinasema kuwa waendeshaji wote 600 akiwemo Froome, ambaye alibadili uraia kutoka Kenya na kuwa Muingereza mwaka 2008, pamoja na wafanyakazi walipimwa. “Ripoti zinasema hakuna yeyote alipatikana ameambukizwa virusi hivyo,” tovuti ya Cycling Weekly imesema.

“Tunapatia usalama kipaaumbele,” Baraza la Michezo la Abu Dhabi walisema.

Mwanzoni baraza hilo lilisema kuwa watu wawili waliokuwa wagonjwa walikuwa “washiriki” katika mashindano hayo. “Wafanyakazi wawili wa Waitaliano wa timu moja inayoshiriki UAE Tour wamepatikana na virusi vya Coronavirus,” UAE Tour ilisema kwenye mtandao wa Twitter baadaye.

“Tumechukua hatua hizo kuhakikisha washiriki wote wako salama.” Yates aliongoza mashindano baada ya mkondo wa tano kabla ya timu na waendeshaji baiskeli kutangaza baadaye Alhamisi kuwa yamefutiliwa mbali.

“Ni aibu kuwa mashindano ya UAE Tour yamefutiliwa mbali, lakini ni jambo la busara kutilia maanani afya ya umma kwanza,” alisema Froome,34, katika mtandao wake wa Twitter. “Tunasubiri kupimwa na tutasalia katika hoteli yetu mpaka tupate taarifa zaidi,” alisema Froome, ambaye alikuwa anarejea mashindanoni baada ya kuumia miezi minane iliyopita katika mashindano ya kifahari ya Tour de France nchini Ufaransa mwezi Juni 2019.