Michezo

Virusi vyasababisha China kusimamisha soka yake yote

January 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

BEIJING, China

CHINA ilitangaza Jumatano imesimamisha mashindano yote ya soka nchini humo pamoja na kuahirisha Ligi Kuu kwa muda usiojulikana kufuatia mkurupuko wa virusi hatari; coronavirus.

Ligi Kuu ya msimu 2020 iliratibiwa kung’oa nanga Februari 22, lakini imeahirishwa pamoja na aina zote za mechi za soka ili shughuli za kukabiliana na virusi hivyo zitapate kuendeshwa na kudhibiti ugonjwa wa nimonia.

Tangazo hilo kutoka kwa Shirikisho la Soka nchini China lilitolewa saa chache baada ya Riadha za Dunia za Ukumbini zilizoratibiwa kufanyika mjini Nanjing mwezi Machi kuahirishwa hadi mwaka 2021 kufuatia ushauri wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Soka ina ufuasi mkubwa katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu duniani, huku klabu tajiri zikiajiri wachezaji ghali wa kigeni kama raia wa Brazil Hulk na Oscar, na raia wa Argentina Carlos Tevez katika miaka ya hivi karibuni.

Kufikia Alhamisi, virusi hivi vilikuwa vimeua watu 170 nchini China pamoja na visa 7,700 kuripotiwa.

Virusi vimeenea katika zaidi ya mataifa 15 barani Asia, Ulaya, Amerika ya Kaskazini na pia Mashariki ya Kati.