Michezo

Vishale: Nairobi Stima na Trans Nzoia zaanza vyema

July 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

TIMU za Nairobi Stima na Trans-Nzoia zimetwaa uongozi wa mapema katika vishale ya Ligi Kuu ya Kenya Darts Association (KDA) baada ya kila moja kuvuna alama 15 kwenye mechi zilizochezewa ukumbi wa Florida Inn Hall, Ngong Town Kaunti ya Kajiado.

Magereza na Machakos County zilivuna alama 13 na 12 mtawalia huku bingwa mtetezi Mang Darts ikizoa alama kumi.

Warusha vishale wa Nairobi Stima walianza vyema walipozaba Mang Darts alama 8-2 kisha kuzoa pointi 7-3 mbele ya Museum.

Mang Darts ilifikisha alama kumi ilipotandika Loitoktok 8-2. ”Mang Darts tuliteleza na kukosa maarifa mbele ya Nairobi Stima lakini tunapania kurekebisha makosa yetu kwenye mechi sijazo,” mchezaji wa Mang, Wycliffe Omariba alisema.

Nao Peter Mwenda(Meru) na Nahum Munyao (Machakos) walibeba taji la Florida Cup kwenye mechi za mchezaji mmoja (singles) baada ya kutesa katika fainali ya wanaume na wanawake mtawalia.

Peter Mwenda alizaba William Mbogo (Nairobi Stima) seti 5-4 wakati Nahum Munyao akibugiza Selina Sakawa wa Tume ya Mamlaka ya Mawasiliano (CAK) kwa seti 5-2.

Nao Peter Wanjie wa APTC (wanaume) na Pascaline Mueni wa Mang (wanawake) waliibuka wafungaji bora walipopiga alama 180 mara sita na 180 mara tatu kitengo cha wanaume na wanawake mtawalia.

Kwenye nusu Peter Mwenda alicharaza James Mwang i(Museum) seti 4-0 naye William Mbogo alishinda Michael Njuki (Embu) seti 4-2. Kwa wanawake, Nahum Munyao alichoma Rosemary Wangui (Blue Triangle) seti 4-1 naye Selina Sakawa alivuna seti 4-2 dhidi ya Loveth Chumba (Magereza).