Michezo

Vision yalenga kushiriki ligi ya daraja ya pili msimu ujao

June 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

NI kati ya vikosi vinavyopitia pandashuka nyingi tu ili kuendeleza mpango wake kushiriki mechi za Kanda A kuwania taji la Nairobi East Regional League (NERL) imeibuka kati ya vikosi vinavyokuja kwa kasi msimu huu. Vision FC iliyoanzishwa miaka 19 iliyopita ina vijana wenye vipaji vya kugaragaza gozi ya ng’ombe.

Wachezaji wa kikosi hiki chini ya kocha mkuu, Edwin Kanyonyi akisaidiana na Willis Odhiambo wakiingia mjegoni huonyesha ujuzi tosha kwa kusakata soka safi.

Kwenye mechi za ngarambe hiyo wanaoshiriki kwa mara ya kwanza hakika wanatesa wapinzani wao si haba. ”Bila kujipigia debe tumepania kujitahidi kadiri ya uwezo wetu tufuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu ujao,” kocha mkuu anasema na kuongeza kuwa udhamini ndiyo tatizo kubwa. Anatoa mwito kwa wahisani wajitokeze pia washirikiane na timu za mashinani kwenye juhudi za kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.

Vision FC ya mtaani Mukuru Kwa Njenga imeibuka kati ya timu tano zinazowasha moto mkali kwenye mechi za kipute hicho msimu huu. Kocha huyo anasema kwa sasa wamekaa pazuri kujituma ili kumaliza kidedea na kutwaa tiketi ya kusonga mbele.

”Tumebakisha mechi nne ili kukamilisha ratiba yetu ambapo patashika zote tunacheza kama fainali. Tumeshangaza wapinzani wengi baada ya kupepeta Mbotela Kamaliza FC mabao 2-1 kisha kuvuna idadi sawa na hiyo dhidi ya Nairobi Water FC juzi Jumapili,” alisema.

Kwenye kampeni za kipute hicho, Vision FC inakabiliana bega kwa bega na Uprising FC, Mbotela Kamaliza FC bila kusahau Creative Hands FC.

Kwenye jedwali, Uprising inaongoza kwa alama 33, mbili mbele ya Mbotela Kamaliza baada ya kucheza mechi 18 na 17 mtawalia. Nao wanasoka wa Vision FC wamefunga tatu bora kwa kuzoa alama 28, moja mbele ya Creative Hands FC huku Nairobi Water ikitinga nafasi ya tano kwa alama 24 sawa na Sofapaka Youth tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Kati ya wachezaji wake Jonadhan Nzuki ambaye mara kwa mara hubeba mzigo wa kikosi hicho anadai hawana la ziada mbali watapanda ngazi.

”Tumeamini katika mitaa ya chini kunazo vipaji nyingi tu ila huwa vigumu kutambuliwa,” alisema na kuongeza wamepania kutinga Ligi Kuu ndani ya miaka mitano ijayo. Anatoa mwito kwa mawakala wa klabu za Ligi Kuu nchini wawe wanateremka mashinani kusaka wachezaji wenye vipaji.

Vision FC inajumuisha:Aggrey Ochieng, Ihaji Mulovi, Daniel Mutiso, Benson Omwami, Moses Kithusi, Billy Otinori, Benjamin Wanyonyi, James Muema, Kenneth Odhiambo, Brian Nyabuto, Jonathan Nzuki, Kevin Ouma, Ignacio Shavasinya, Wycliffe Muhonja, Flerious Mbatha na Rodgers Wafula. Wengine ni Eugyne Mukangula, Julius Omondo, Wycliffe Oyugi, Nicholas Wambua, Julius Oseko, Gaddafi Nyabuto, Ali Musindalo, Denis Weru, Alex Mbondo, Dominic Ndunda, Dennis Ochieng, Joseph Mbuvi, David Gayo na Josphat Marocha.