Wabunge waitaka serikali kujenga viwanja 8 vya hadhi nchini
Na CHARLES WASONGA
HATIMAYE wabunge ambao walisafiri hadi nchini Urusi kutizama mchuano wa Kombe la Dunia Alhamisi waliwasilisha ripoti yao bungeni, wiki mbili baada ya Spika Justin Muturi kuwashinikiza kufanya hivyo.
Ziara hiyo ambayo iliibua kero miongoni mwa Wakenya wa matabaka mbalimbali ilifadhiliwa kwa Sh25 milioni, pesa za umma. Gharama hiyo ilijumuisha nauli, vyakula, malazi na marupurupu ya wabunge 17 waliokuwa katika ujumbe.
Wananchi walikasirika pale viongozi hao walipoweka picha zao katika mitandao ya kijamii zilizowaonyesha wakijivinjari na mashabiki waliohudhuria mashindano hayo.
Kwenye ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo na Utamaduni Victor Munyaka inaitaka serikali kujenga angalau viwanja vinane vya michezo vya kisiasa ili kuiwezesha Kenya kuandaa michezo ya hadhi ya kimataifa siku zijazo.
“Kenya imekuwa ikipoteza nafasi ya kuandaa mashindano mbalimbali ya michezo ya kimataifa kwa sababu ya ukosefu wa viwanja. Hii ndio maana kamati hiii inaitaka serikali kupitia wizara ya michezo kujengo viwango katika mikoa nane ya zamani,” akasema Mbunge huyo wa Machakos Mjini.
Kamati pia inapendekeza kwamba viwanja vya michezo vya Kasarani, Nyayo, Machakos, Kipchoge Keino na Kinoru, vipandishwe hadhi hadi kufikia viwango vinavyohitajika na Shirikisho la Kandanda Ulimwenguni (FIFA).
“Viwanja vya michezo nchini Urusi vimejengwa kwa ubora wa juu zaidi. Hii ndio maana tunapendekeza kuwa viwanja viwango vitano ambako Kandanda ya Mataifa ya Afrika (CHAN) huandaliwa viboreshwe zaidi,” Bw Munyaka akasema.
Ripoti hiyo pia inaitaka Wizara ya Michezo kuanzisha na kustawisha vituo vya kukuza talanta za wanamichezo chipukizi (Sports Academies).
“Vituo vya kukuza talanta vinapasa kuanzishwa katika kila moja ya maeneo bunge yote 290 ili kukuza talanta miongoni mwa vijana kuanzisha ngazi za mashinani. Vilabu vya soka pia vinapaswa kuanzisha vituo hivyo vya kukuza talanta za miongoni mwa vijana.” inapendekeza ripoti hiyo.
Wabunge hao pia wanaitaka serikali kuipa ufadhili wa kutosha timu ya kitaifa Harambee Stars ili iweze kunawiri na kushiriki katika makala yajayo ya Kombe la Dunia nchini Qatar.
Kinaya ni kwamba Wiziri wa Michezo Rashid Echesa ambaye anafaa kuongoza utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Dkt Munyaka, alipuuzilia mbali ziara ya wabunge hao akisema haikuwa na maana yoyote.
Hii ni kwa sababu, akasema, wacheza wa Harambee Stars, Maafisa wa Wizara yake au wale wa Shirikisho la Kandanda Nchini (KFF) hawakupewa nafasi kwenda Urusi.