Michezo

Wachezaji wa Gor wanaolalamika watakiwa kujituma

February 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

WACHEZAJI wa Gor Mahia wametakiwa kujituma katika kila mechi badala ya kulalamika kwamba kocha Hassan Oktay anapendelea baadhi yao anapotaja kikosi chake.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Omondi Aduda amesikitikia tabia ya wachezaji watajika wa K’Ogalo kulalamika kwamba hawajibishwi uwanjani ilhali hawafanyi bidii ili kurejelea ubora wao wa awali.

“Kwa sasa ushindani ndani ya Gor Mahia ni mkali sana na ni wale wanaojivunia fomu nzuri tena ya kutisha watakuwa wakipangwa na kocha katika mechi za ligi na bara Afrika(CAF),” akatanguliza Aduda

“Tabia ya baadhi yao kulalamika wanapolishwa benchi na wanaofanya vizuri kuvimba kichwa kiasi cha kutoambiliwa na kutosemezewa itawaharibia taaluma yao ya soka. Wanafaa kuwa na subira, heshima na bidii uwanjani ili kupata nafasi katika kikosi cha kwanza,” akaendeleza Aduda.

Timu hiyo imeshudia mabadiliko makubwa kikosini baada ya kusajiliwa kwa Dennis Oliech na kupanda kwa kiwango cha soka ya baadhi ya wachezaji waliokuwa wakilishwa benchi hapo awali.

Winga George ‘Black berry ’ Odhiambo amelazimika kusugua benchi na nafasi yake kutwaliwa na Boniface Omondi huku ujio wa Oliech na kung’aa kwa Nicholas Kipkirui, kukiwatia pabaya Francis Mustafa, Bernard Ondiek na Erisa Ssekisambu katika safu ya shambulizi.

Katika safu ya kiungo, Kenneth Muguna baada ya kulalamika na kutishia kuondoka K’Ogalo majuma machache yaliyopita amerejelea ubora wake na amekuwa akipangwa na Oktay katika nyingi za mechi zilizopita.

“Nawaomba wanaolalamika watumie Muguna kama kielelezo bora ili wafahamu kwamba watacheza tu ikiwa wanamridhisha kocha wakati wa vipindi vya mazoezi,” akasisitiza Aduda wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali.