• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Wachezaji wa Oyugis FC waamini ipo siku watacheza soka ya kimataifa

Wachezaji wa Oyugis FC waamini ipo siku watacheza soka ya kimataifa

NA RICHARD MAOSI

Mchezo wa soka ndio wenye umaarufu mkubwa duniani huku mashabiki wakipigia upatu timu zao za nyumbani kutwaa ushindi kila mechi. 

Soka mbali na kuwa njia ya kutoa burudani pia imewaajiri watu wengi sana duniani,pamoja na kuwaunganisha raia wa kila rika,rangi na matabaka.

Kandanda imekuwa na washiriki wengi ambao ni wa jinsia ya kiume lakini miongoni mwa akina dada ushabiki ni mdogo mno

Lakini FIFA imetoa nafasi kubwa na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye michezo na hata,ikabuni ligi za akina dada zinazoshindania mataji sawia na timu za wanaume.

Mojawapo ni timu ya wasichana ya SEP OYUGIS FC (Society Empowerment Project) kutoka Oyugis inayoshiriki ligi ya divisheni ya kwanza nchini almaarufu kama Super League.

Mkufunzi George Osoya anasema kikosi chake ni dhabiti,na kinawaleta pamoja mabinti kutoka familia maskini lakini wenye kipaji cha kusakata kabumbu.

Alianzisha SEP Oyugis mnamo 2011 ili kuwaleta pamoja wachezaji wenye maono na kuwashughulisha mabinti baada ya kuhitimisha masomo ya kidato cha nne.

Aliona haja ya wao kupata mwelekeo maishani wasije wakapoteza dira kutokana na wimbi la vijana linalochangia mimba za mapema, na utumiaji wa mihadarati.

Kila siku za wiki kuanzia siku ya Jumatatu hadi Ijumaa, SEP hufanya mazoezi yao kunyosha viungo kwenye uwanja wa Kotieno Primary School inayopatikana mjini Oyugis.

Anasema walianzia ligi za daraja za chini lakini ukakamavu na bidii za wachezaji wake ,zilimfungulia njia akalenga mbali zaidi baada ya kupiku timu pinzani kwa urahisi.

Anasema mnamo 2013 akishiriki ligi ya daraja la pili alifika fainali na kunyanyua taji lililompatia nafasi ya kushiriki divisheni ya kwanza (National Division One).

“Ligi za wanawake kote nchini zina changamoto nyingi, mojawapo ikiwa ni ukosefu wa ufadhili au matatizo ya kuratibu na kuendesha ligi,”Osoya akasema.

Kwa upande wake anaona itakuwa ni jambo la manufaa endapo wadhamini zaidi watajitokeza kupiga jeki ligi za akina dada humu nchini.

Alieleza kuwa licha ya timu nyingi kufanya vyema ligini au kwenye mashindano ya daraja la juu, wasichana wengi wamekuwa wakiagana na soka kwa sababu ya ukosefu wa mtu wa kuwtia moyo waendelee kucheza.

Timu ya akina dada SEO Oyugis inayoshiriki michuano ya divisheni , ligi ya kwanza FKF imeendeleza wimbi a matokeo mazuri kwenye kampeni yake kusaka nafasi ya kujiunga na ligi ya akina dada nchini Women Premier League (WPL).

Mkufunzi Osoya anaamini ifikapo 2020 kikosi chake kitakuwa tayari katika kampeni ya kutifuana vumbi na timu nyinginezo nchini zilizokubuhu ligini.

Mkufunzi anasema wachezaji wake wameshinda mechi zao zote ya punde ikiwa ni baina yao na Bunyore Ladies, ambapo waliwabamiza 1-0, wiki mbili zilizopita.

Nahodha wa kikosi Lavenda Kiako anasema ili kufikia viwango vya kimataifa kwa timu ya SEP Oyugis kuandikisha matokeo mazuri,ndiyo siri.

Aidha katika pambano la awali walinyamazisha Gusii Starlets FC 3-2 ugenini.

“Wachezaji wetu ni wazoefu hasa ijapo katika ligi za daraja la juu,nina uhakika kuwa watajituma na bidii zao zitazaa matunda,kwa kuandikisha matokeo mazuri,”Kiako akasema.

Wikendi liyopita ingawa walipoteza 6-0 dhidi ya Nakuru West Queens,wamejinyanyua na kufanya marekebisho madogo katika kikosi.

Wameimarisha safu ya ulinzi na ile ya mashambulizi wakihemea huduma za wachezaji nguli kutoka Nakuru Queens kama vile Diana Kosgei ambaye kufikia sasa anaongoza kwenye idadi ya ufungaji magoli.

“Mpango wetu sasa ni kunasa saini za makinda wenye vipawa ili waje kuisaidia timu kufana,”akasema.

Kikosi cha SEP Oyugis mbali na kufanya kazi za jamii wamekuwa wakishirikiana na wakazi wa Kasipul kusafisha jiji, kama njia ya kurudisha shukran kutokana na ushabiki wa dhati.

Wachezaji wengi hapa wanaamini kuwa siku moja watacheza soka ya kulipwa katika kiwango cha kimataifa.

Mkufunzi Osoya hata hivyo anawashauri wazazi kutupilia mbali dhana potovu kuwa soka ni ya wanaume tu.

Pia anawahimiza kukumbatia vipaji vya watoto wao wakiwa wachanga kwa sababu vinaweza kuwafikisha mbali siku moja.

“Michezo ni njia nyingine itakayosaidia kutengeneza nafasi nyingine za ajira bila kutegemea zile haba zinazopatikana ofisini,” alisema.

You can share this post!

Tuliamka asubuhi kukuchagua lakini umetusaliti, Waititu...

Je, ushirikina husababisha ajali za barabarani?

adminleo