Wachezaji wa Roma wakubali kujinyima mshahara kwa miezi 4 kusaidia klabu
Na CHRIS ADUNGO
AFISA mkuu mtendaji wa AS Roma, Guido Fienga, amewamiminia sifa wachezaji wake kwa utu wa kujinyima mishahara kwa kipindi cha miezi minne ijayo ili kusaidia klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) katika kipindi hiki kigumu cha janga la corona.
Wachezaji wote na maafisa wa benchi ya kiufundi inayoongozwa na kocha Paulo Fonseca pia watatoa sehemu ya hazina zao binafsi za fedha kwa minajili ya kuwadumisha kimishahara baadhi ya wafanyakazi na vibarua wa klabu hiyo.
Hatua ambayo imechukuliwa na wachezaji wa Roma ni zao la majadiliano ya kina kati ya nahodha Edin Dzeko, kikosi kizima na kocha Fonseca ambao wametaka maamuzi hayo kutekelezwa kaunzia mwisho wa mwezi huu.
“Sisi husisitiza sana masuala yanayohusu umuhimu wa umoja ndani ya kikosi cha Roma. Kujitolea kujinyima mshahara kwa miezi minne na kukatwa asilimia 30 ya ujira wao hapo baadaye hadi corona itakapodhibitiwa vilivyo duniani kote ni ishara ya ubinadamu,” akatanguliza Fienga.
“Dzeko pamoja na wachezaji wenzake na kocha wao wamedhihirisha kwamba wanaelewa maadili na misingi ya kubuniwa kwa kikosi cha Roma. Tunawashukuru pakubwa kwa ukarimu utakaowawezesha vibarua wetu wote kuhifadhi kazi zao kikosini,” akasema kinara huyo.
Roma hawajawahi kusakata mchuano wowote tangu Machi 1, siku chache kabla ya kipute cha Serie A kusitishwa kwa muda kutokana na mlipuko wa virusi vya homa kali ya corona.
Katika barua yao kwa Fienga, wachezaji wa Roma walisema: “Tuko tayari kurejea uwanjani haraka iwezekanavyo na kutoa chote tulichonacho ilmuradi tuyafikie malengo yetu kama klabu. Ingawa hivyo, tunatambua kwamba hatua yetu hii ni mchango mdogo sana usioweza kutatua kabisa matatizo makubwa ya kiuchumi ambayo yameletwa na corona.”
“Kwa kuongozwa na moyo wa kusaidia klabu iendelee kusimama na kuwa ya msaada kwa wengi wanaoitegemea, tunapendekeza hatua hii ya kifedha kwa mishahara yetu kutekelezwa kuanzia mwisho wa Aprili 2020,” ikasema sehemu ya barua hiyo iliyotiwa saini na masogora wote wa Roma ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama 45, tatu nyuma ya Atalanta wanaofunga mduara wa nne-bora.
Italia ndiyo nchi iliyoathiriwa pakubwa zaidi na virusi vya corona barani Ulaya huku zaidi ya vifo 23,000 vikiripotiwa kufikia Aprili 19, 2020.