Michezo

Wachezaji wazoefu wanaangusha kikosi – Arteta

December 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal amewataka mashabiki wa kikosi hicho kuvuta subira zaidi kwa matarajio kwamba wanasoka wake watajinyanyua hivi karibuni na kuanza kusajili matokeo ya kuridhisha.

Ingawa hivyo, Arteta ametilia shaka kiwango cha kujitolea kwa baadhi ya wachezaji wake wazoefu, hoja ambayo imeungwa mkono na nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Alan Shearer ambaye anahofia kwamba huenda Arsenal watateremshwa daraja mwishoni mwa kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu.

Kichapo cha 2-1 ambacho Arsenal walipokezwa na Everton mnamo Disemba 19 kilifanya Arsenal ambao sasa wamepoteza mechi nane kati ya 14 zilizopita, kuweka rekodi ya mwanzo mbaya zaidi ligini tangu 1974-75.

Kichapo hicho kilisaza Arsenal ya kocha Mikel Arteta katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 14 pekee.

Masaibu ya Arteta na Arsenal huenda sasa yakaongezeka zaidi katika kipindi cha wiki moja ijayo ikizingatiwa kwamba wana kibarua kigumu dhidi ya Manchester City katika robo-fainali za Carabao Cup mnamo Jumatano ya Disemba 23 kabla ya kualika Chelsea kwa gozi la EPL wikendi hii.

“Haya ni matokeo yasiyokubalika. Haiwezekani kabisa kwa kikosi kuangushwa mara kwa mara na wachezaji wazoefu wasiojituma jinsi inavyotakikana,” akasema Arteta katika kauli iliyolenga kumrejelea beki Rob Holding aliyejifunga dhidi ya Everton.

“Tunahitaji kujituma zaidi na kuanza kushinda mechi. Ushindi utatuaminisha kufanya vyema. Lakini huu ni wakati ambapo wachezaji wazoefu wanastahili kusimama na kikosi na kuwa kielelezo kwa chipukizi wetu,” akaendelea kocha huyo raia wa Uhispania ambaye pia amewahi kuchezea Everton na Arsenal.

Ingawa hivyo, Shearer amesema “hana uhakika iwapo Arsenal wataponea ligini muhula huu iwapo Arteta ataendelea kutegemea kikosi chenye baadhi ya wanasoka wasiojituma na wasioongozwa na uzalendo.”

“Kinyume na Liverpool, Tottenham, Man-City na Man-United ambao wameonyesha ari ya kushinda ligi na kuweka wazi maazimio yao ya msimu, Arsenal hawana motisha yoyote na ni kama wanacheza kwa kujilazimisha tu,” akasema Shearer.

Kichapo kutoka kwa Everton kiliwaning’iniza Arsenal pembamba kiasi kwamba kwa sasa ni alama nne pekee ndizo zinazowadumisha nje ya mduara wa vikosi vitatu vya mwisho vinavyokodolea macho hatari ya kushushwa ngazi.

Kubwa zaidi linalotatiza Arsenal ni utovu wa nidhamu miongoni mwa wanasoka wazoefu na ubutu wa mafowadi ambao hawajawahi kufunga bao lolote la kawaida isipokuwa kupitia penalti kutokana na mechi tano zilizopita za EPL ugenini.

Bao lililopachikwa wavuni na Nicolas Pepe dhidi ya Everton lilikuwa lake la pili ligini msimu huu na lilitokana na penalti sawa na la kwanza msimu huu.

“Arsenal walikuwa ovyo dhidi ya Everton. Kikosi kilikosa ubunifu na baadhi ya masogora hawakutia bidii wala kuonyesha nia ya kucheza kwa kujitolea na kuwakabili wapinzani,” akasema Shearer.

“Mikel Arteta anastahili kuwa na kila sababu ya kuhofia kazi yake. Hawezi kuendeleza kutegemea wachezaji waliopo kwa sasa kambini. Yasikitisha kwamba Arsenal wamefunga mabao 12 pekee kutokana na mechi 14.”

“Pepe alionekana tu akijivuta uwanjani akitembea. Kwa mchezaji wa kiwango chake na ambaye anatarajiwa kubeba kikosi, hilo ni jambo la kutisha. Hakuna wakati ambapo alikuwa amejiandaa kuingia ndani ya kijisanduku cha Everton na hakuna mchezaji wa Arsenal aliyeonyesha kutawaliwa na kiu ya kufunga mabao.”

“Wapo wachezaji wachache wa Arsenal ambao hawataki kuwajibika na kumpiga jeki kocha wao. Ni aibu kwa sababu Arsenal hawatafunga mabao iwapo wataendelea kucheza hivyo,” akaongeza jagina huyo wa soka aliyewahi kuvunja rekodi nyingi akivalia jezi za Newcastle United (1996-2006).

Arsenal waliokosa huduma za fowadi na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang, waliponea chupuchupu kufungwa mabao mengi ya mapema huku sajili mpya Willian Borges aliyetokea Chelsea mwishoni mwa msimu wa 2019-20, akishindwa tena kutamba.

Utovu wa nidhamu ambao umekuwa ukiandama Arsenal katika mechi kadhaa zilizopita bado ulidhihirika dhidi ya Everton baada ya Dani Ceballos aliyeponea kuonyeshwa kadi nyekundu kumchezea visivyo kiungo Yerry Mina.

Mbali na Pepe aliyeonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Leeds United, wachezaji wengine wa Arsenal waliowahi kuonyeshwa kadi nyekundu hivi karibuni kwa utovu wa nidhamu ni kiungo Granit Xhaka na beki Gabriel Magalhaes.

Japo ushindi wa Kombe la FA mwishoni mwa msimu uliopita na wa Community Shield mwanzoni mwa muhula huu uliashiria ufufuo wa Arsenal chini ya Arteta, kikosi hicho sasa kimepiga jumla ya mechi saba za EPL bila ya kusajili ushindi wowote.

Holding anakuwa sasa sogora wa tatu wa Arsenal kujifunga katika EPL msimu huu baada ya Bukayo Saka dhidi ya Aston Villa na Aubameyang dhidi ya Burnley.