• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
WAFALME! Man-City wabeba kombe kwa mara ya 3 mfululizo

WAFALME! Man-City wabeba kombe kwa mara ya 3 mfululizo

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

TIMU ya Manchester City ilitwaa taji la Carabao Cup kwa mara ya tatu mfululizo, ilipowatandika Aston Villa 2-1 katika uwanja wa Wembley, Uingereza, siku ya Jumapili.

Mvamizi Sergio Aguero na kiungo Rodrigo Hernandez walifunga mabao ya Man-City kunako dakika za 20 na 30 kabla ya Mbwana Samatta kuwafutia Villa machozi mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Zaidi ya mataji matatu ya League Cup, Guardiola anajivunia pia kuwaongoza Man-City kunyanyua mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), ubingwa mmoja wa Kombe la FA na mataji mawili ya Community Shield.

“Tangu tuanze kushinda, tumetia kapuni mataji manane kati ya tisa yaliyopita katika soka ya Uingereza. Hili ni jambo la kutia fora mno. Sidhani kwamba pana kikosi chochote kingine katika historia ya mapambano ya soka ya Uingereza ambacho kimewahi kufikia mafanikio haya,” akatanguliza Guardiola.

Akaongeza: “Hata Liverpool iliyotamba katika miaka 80 haikuweza kufikia ufanisi huu tunaojivunia sasa. Man-United ya Sir Alex Ferguson, Chelsea ya Jose Mourinho na Arsenal ya Arsene Wenger pia zilishindwa.”

Man-City ni kikosi cha pili baada ya Liverpool kunyakua ubingwa wa League Cup mara tatu mfululizo. Liverpool walifanikiwa kufanya hivyo kwa misimu minne mnamo 1980-81 na 1983-84.

Ni Liverpool pekee ambao wametawazwa mabingwa wa kipute hicho mara nyingi zaidi (mara nane) kuliko Man-City ambao wameibuka mabingwa katika jumla ya misimu saba.

Liverpool walitia kibindoni mataji sita ya EPL, mawili ya Kombe la FA na manne ya League Cup katika miaka ya 80.

Kwa upande wao, Man-United walinyanyua mataji 13 ya EPL, yakiwemo matatu mfululizo katika vipindi viwili tofauti chini ya kocha Ferguson. Kwa upande wake, Wenger aliwahi kuwaongoza Arsenal kutawazwa mabingwa wa EPL bila ya kupoteza mchuano wowote katika msimu wa 2003-04.

Guardiola aliyejiunga na Man-City mnamo 2016, aliwaongoza waajiri wake hao kutwaa jumla ya mataji matatu ya EPL, FA na League Cup msimu jana baada ya kunyakua pia ubingwa wa Community Shield mwanzoni mwa muhula huo.

Japo amekiri kwamba itakuwa vigumu zaidi kwa vijana wake kuwania ufalme wa EPL msimu huu hasa ikizingatiwa ukubwa wa pengo la alama kati yao na Liverpool, Guardiola amesisitiza kuwa vijana wake wana uwezo wa kunyanyua makombe mawili zaidi – FA na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mwanzoni mwa Februari 2020 Guardiola alikiri kwamba atakuwa amefeli pakubwa iwapo atabanduka uwanjani Etihad bila ya kuwaongoza waajiri wake Man-City kutia kapuni taji la UEFA.

“Mwaka 2019 ulikuwa bora zaidi kwa Man-City. Licha ya ufanisi wa kutetea ubingwa wa EPL, mashabiki walihisi kutoridhishwa na tukio la kikosi kutonyakua ufalme wa UEFA,” akasema Mhispania huyo ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Chini ya Guardiola aliyetua Etihad mnamo 2016, Man-City hawajawahi kupita hatua ya robo-fainali ya UEFA na matumaini yao ya kusonga mbele yalizimwa na Monaco, Liverpool na Tottenham kwenye awamu ya nane-bora katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita.

“Man-City kwa sasa ni kikosi cha haiba kubwa ambacho kina uwezo wa kutishia mpinzani yeyote katika soka ya bara Ulaya. Zamani, isingekuwa rahisi kwa kikosi hiki kuenda Uhispania na kuwapiga Real katika mechi ya UEFA,” akasema Guardiola ambaye kwa sasa anakiandaa kikosi chake kumenyana na Sheffield Wednesday katika raundi ya tano ya Kombe la FA hapo kesho Jumatano ugani Hillsborough.

Baadaye, mabingwa hao watetezi wa taji la EPL wameratibiwa kuchuana na Man-United na Burnley ligini kabla ya kurudiana na Real katika gozi la UEFA uwanjani Etihad.

Kwa upande wao, Villa watatoana jasho na Leicester City mnamo Jumatatu ijayo kabla ya kukwaruzana na Chelsea, Newcastle, Wolves na Liverpool kwa usanjari huo.

  • Tags

You can share this post!

Real Madrid yagaragaza Barca katika El Clasico

Mkutano wa BBI Eldoret wafutwa

adminleo