Michezo

Wajir All Stars, Wajir Queens mabingwa wa Safaricom Chapa Dimba Kaskazini Mashariki mwa Kenya

February 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA TOTO AREGE

WAJIR All Stars ndio mabingwa wa Safaricom Chapa Dimba Kanda la Kaskazini Mashariki mwa Kenya, baada ya kuinyoa Lyon 04 FC kutoka kaunti ya Garissa 2-0 katika fainali iliyopigwa Jumapili, Februari 25, 2024 katika Chuo Kikuu cha Garissa.

Mshambulizi Mohammed Adan alicheka na wavu wa kwanza dakika ya 35 kabla ya Mursal Abdinasir kufunga bao la pili dakika ya 70.

Lyon wangepata bao la kusawazisha dakika ya 56 kupitia mkwaju wa penalti lakini Yahye Abdikadir alikosa kulenga shabaha ambapo, mlinda lango wa Wajir Mohamed Noor Faizal alipangua shuti hilo.

Wajir sasa itawakilisha Kanda ya Kaskazini Mashariki katika fainali ya kitaifa ya Chapa Dimba ambayo itaandaliwa  Kaunti ya Kisumu Aprili 2024.

Kando na timu hiyo ya wanaume, Wajir Queens pia ilifuzu kucheza fainali.

Chini ya uongozi wa  kocha Ahmed Mohamed Abdullahi, walitawazwa mabingwa wa kikanda baada ya kuizidi nguvu Wajir Starlets 2-0 mapema mwezi huu (Februari 2024) katika michezo yao ya mkoa.

All Stars na Wajir Queens zimejishindia Sh250,000 kila mmoja pamoja na vikombe na medali.

Washindi wa pili, Lyon 04 FC, pia walienda nyumbani na Sh150,000 kila mmoja.

Mchezaji Bora wa Mchezo (MVP), Kipa Bora, na Mfungaji Bora (wavulana na wasichana) kila mmoja alipokea Sh30,000.

Mbali na pesa, kila mchezaji alijishindia simu.

Washambulizi bora Mohamud Adan na Abdinasir Mursal kutoka All Stars walituzwa Sh 30,000 pamoja na mlinda lango Nur, Mchezaji bora wa mashindano Hussein Yusuf Hussein kutoka Lyon FC, wakienda nyumbani na kiasi sawa na hicho.

Wanaungana na timu za Ebwali FC na Brenda Girls kutoka Magharibi mwa Kenya, Obunga FC na Plateau Queens (Nyakach Girls), PASC Langa na Wiyeta Girls kutoka Bonde la Ufa, Chuka Scorpions na Syomunyu Secondary kutoka Mkoa wa Mashariki, na Bandari Youth na Changamwe Ladies kutoka Mkoa wa Pwani ambao tayari wamefuzu kwa fainali za kitaifa.

Mwaka huu, mashindano ya Safaricom Chapa Dimba katika eneo la Kaskazini Mashariki yalishirikisha jumla ya timu 286 kutoka kaunti sita za eneo hilo ikiwa ni pamoja na: Mandera (115), Garissa (60) na Wajir (111).

Mashindano haya yanakusudia kutoa jukwaa imara kwa wachunguzi na makocha kutambua vipaji vipya na kujenga mifumo ya kuendeleza ligi za soka nchini Kenya wakati pia ikiwapa mafunzo jumla ya makocha 250.

Mashindano haya yanalenga wachezaji wa soka wenye umri kati ya miaka 16 na 20.

Baada ya mashindano ya Kaskazini Mashariki kukamilika, Chapa Dimba inaelekea jijini Nairobi, ambapo timu nane zitapigania tiketi ya kucheza katika fainali.