Michezo

Wakenya 5 kuwania mataji ya kimataifa katika riadha

October 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

WAKENYA wanapigiwa upatu wa kutamalaki tuzo za Wanariadha Bora wa Mwaka duniani katika hafla itakayoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) mnamo Novemba 23, 2019 jijini Monaco, Ufaransa.

Wakenya Brigid Kosgei, Beatrice Chepkoech na Hellen Obiri wameorodheshwa kuwania taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake huku Eliud Kipchoge na Timothy Cheruiyot wakiunga orodha ya watimkaji watakaopigania tuzo hiyo kwa upande wa wanaume.

Kosgei alitiwa katika orodha hiyo baada ya kuvunja rekodi ya dunia kwa upande wa marathon ya wanawake mwishoni mwa wiki iliyopita alipoboresha muda wa zamani uliodumu kwa kipindi cha miaka 16 kwa zaidi ya dakika moja.

Nyota huyo alikamilisha mbio za Chicago Marathon, Amerika kwa muda wa saa 2:14.04 mnamo Jumapili iliyopita na kuondoa dakika moja na sekunde 21 kutoka kwa rekodi iliyowekwa na Mwingereza Paula Radcliff mnamo 2003.

Chepkoech ndiye bingwa wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji. Zaidi ya kutia kapuni ubingwa wa mbio za Diamond League msimu huu, alitawala mashindano saba kati ya manane aliyoyashiriki mwaka huu. Muda wa dakika 8:57.84 aliouandikisha katika Riadha za Dunia zilizokamilika majuzi jijini Doha, Qatar ulimvunia nishani ya dhahabu.

Kiini cha kuteuliwa kwa Obiri ni ufanisi aliojivunia katika Mbio za Nyika za Dunia jijini Aarhus, Denmark mwanzoni mwa mwaka huu kabla ya kunyanyua medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 kwenye Riadha za Dunia za Qatar kwa muda wa dakika 14:26.72. Awali, alikuwa amesajili muda bora wa dakika 14:20.36 aliposhiriki mbio hizo jijini London, Uingereza mnamo 2017.

Obiri, Kosgei na Chepkoech watatoana jasho na Shelly-Ann Fraser-Pryce wa Jamaica ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 100, Mwingereza Katarina Johnson-Thompson (heptathlon) na Sifan Hassan wa Uholanzi ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 na mita 10,000.

Kipchoge aliweka historia mnamo Oktoba 12 kwa kuwa binadamu wa kwanza kuwahi kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya muda wa saa mbili aliposhiriki kivumbi cha INEOS 1:59 Challenge jijini Vienna, Austria.

Bingwa huyo wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika marathon alikamilisha kivumbi cha INEOS 1:59 Challenge baada ya muda wa saa 1:59:40.2.

Cheruiyot alitwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa majuzi jijini Doha, Qatar. Cheruiyot aliyetawazwa bingwa wa Diamond League mnamo 2017, 2018 na 2019, amewahi pia kunyakua nishani ya fedha katika mbio za mita 1,500 wakati Riadha za Dunia zilipoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017.

Wanariadha wengine watakaopania kuwapiku Kipchoge na Cheruiyot ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 800, Donavan Brazier wa Amerika, Mmarekani Christian Coleman ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 100 na Joshua Cheptegei wa Uganda ambaue ni bingwa wa dunia katika mbio za nyika na mita 10,000.