Wakenya Jeptoo na Kotut wasikitika baada ya mbio za Paris Marathon kuahirishwa tena
Na CHRIS ADUNGO
MBIO za Paris Marathon zimeahirishwa hadi Oktoba 17, 2021, huku zile za Paris Half Marathon zikisogezwa hadi Septemba 5, 2021, kutokana na makali ya virusi vya corona.
Makala ya mbio hizo mwaka huu wa 2020 yalikuwa yameratibiwa kufanyika mnamo Aprili 5 kabla ya kuahirishwa hadi Aprili 11, 2021 kisha kuhamishwa tena hadi tarehe hizo mpya ambazo zimefichuliwa na waandalizi.
Bingwa wa zamani wa London Marathon, Priscah Jeptoo ni miongoni mwa wanariadha waliokuwa wameelekeza macho yao kwa kivumbi cha Paris Marathon.
Jeptoo ambaye amerejea kutoka kwenye likizo ya uzazi amesema kwamba alikuwa amekamilisha maandalizi yake kwa minajili ya mbio hizo na tangazo la kuahirishwa kwa mashindano yenyewe ni pigo kubwa.
“Nilikuwa nimepangia kutumia Paris Marathon kujiandaa vilivyo kwa mashindano mengine ya msimu mpya. Hata hivyo, corona kwa sasa imevuruga mipango yangu. Hakuna kingine ninachoweza kufanya ila kusubiri kwa mwaka mwingine mmoja zaidi kabla ya kunogesha mbio hizo za Paris,” akasema Jeptoo ambaye hujifanyia mazoezi yake katika eneo la Kapsabet, Kaunti ya Nandi.
Mwanariadha mwingine ambaye amefichua kwamba mipango yake ya msimu imevurugwa pakubwa baada ya kuahirishwa kwa mbio za Paris Marathon ni bingwa wa kivumbi hicho mnamo 2016, Cyprian Kotut ambaye ni mwanachama wa 2Running Club inayompa hifadhi Jeptoo.
Kotut amekuwa akiuguza jeraha baya la misuli ambalo lilimweka nje ya kampeni zote za msimu huu wa 2019. Hata hivyo, kwa sasa amerejea na alikuwa radhi kutangaza ujio wake wa haiba kwa kutawala mbio za Paris Marathon. Kotut ni kaka mdogo wa bingwa wa zamani wa marathon, Martin Lel.
Raia wa Ethiopia Abrhaw Milaw alitawazwa bingwa wa Paris Marathon mnamo 2019 kwa upande wa wanaume baada ya kusajili muda wa saa 2:07:050. Mwenzake Asefa Mengistu aliambulia nafasi ya pili kwa muda wa saa 2:07:25 huku Mkenya Paul Lonyangata akiridhika na nafasi ya tatu baada ya saa 2:07:29.
Mbio za upande wa wanawake zilitawaliwa na Gelete Burka (2:22:47) mbele ya Waethiopia wenzake Azmera Gebru (2:22:52) na Azmera Abreha (2:23:35).
Isipokuwa London Marathon na Tokyo Marathon, mbio nyinginezo za marathon za haiba kubwa dunani (MWM) zikiwemo zile za New York, Berlin, Boston na Chicago zilifutiliwa mbali kwa sababu ya janga la corona.