Michezo

Wakenya Maritim na Chebitok watawala Barcelona Marathon

March 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE
WAKENYA Anthony Maritim na Ruth Chebitok waliibuka mabingwa wapya wa mbio za Barcelona Marathon nchini Uhispania, Jumapili.

Maritim, ambaye alikamilisha kitengo cha wanaume kwa saa 2:08:08, aliongoza Wakenya Silas Too (2:08:18) na Hillary Kipsambu (2:08:144) kufagia nafasi tatu za kwanza.

Waethiopia Tariku Kinfu (2:09:17), Tsegay Kebede (2:09:17) na Tsedat Ayana (2:09:17) walinyakua nafasi tatu zilizofuata, huku mzawa wa Kenya Benson Seurei, ambaye ni raia wa Bahrain, akiridhika katika nafasi ya saba (2:11:19).

Chebitok alirejesha taji la wanawake ambalo Muethiopia Helen Bekele alitwaa mwaka jana. Alishinda makala ya mwaka huu kwa saa 2:25:49.

Alifuatwa kwa karibu na Waethiopia Belaynesh Tsegaye (2:26:18), Worknesh Alemu (2:27:29) na Alemitu Begna (2:30:54), huku Mkenya Lucy Wanjiku akifunga tano-bora (2:34:53).

Ni mara ya kwanza kabisa Kenya kushinda mataji ya wanaume na wanawake ya Barcelona Marathon tangu ushindi wa Julius Chepkwony na Emily Samoei mwaka 2012.

Rekodi za Barcelona Marathon zinashikiliwa na Mkenya Jackson Kotut (2:07:30) na Bekele (2:25:04), mtawalia.