• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Wakenya wafagia nafasi za kwanza tatu jijini Boston

Wakenya wafagia nafasi za kwanza tatu jijini Boston

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Fancy Chemutai na David Bett wameibuka mabingwa wa mbio za kilomita 10 za Boston (B.A.A. 10k) nchini Marekani mnamo Juni 23, 2019.

Chemutai na Bett, ambao wamejizolea Sh1 milioni kila mmoja, wamekata utepe kwa kukamilisha umbali huo kwa dakika 30:36 na 28:08, mtawalia.

Chemutai alivunja rekodi ya B.A.A. 10k iliyowekwa na Muamerika Shalane Flanagan mwaka 2016 kwa sekunde 16.

Chemutai, ambaye ni mkimbiaji aliye na kasi ya tatu-bora duniani katika kilomita 10, alifuatwa kwa karibu na Wakenya wenzake Brilliant Kipkoech (31:04) na Caroline Rotich (31:58).

Wakimbiaji wengine waliobwagwa na Chemutai ni Betsy Saina, ambaye alishinda Paris Marathon mwaka 2018, Monicah Ngige ambaye aliibuka bingwa wa mbio za kilomita tano za B.A.A mwaka 2018, bingwa mara mbili wa zamani wa B.A.A. 10k Mamitu Daska na mshindi wa mataji ya kilomita 20 na kilomita 21 ya Marekani, Aliphine Tuliamuk.

Katika kitengo cha wanaume, Bett alifuatwa sekunde moja nyuma na Mkenya Daneil Chebii, huku Mkenya mwingine Stephen Sambu akifunga mduara wa tatu-bora (28:11).

Nambari mbili na tatu katika vitengo vyote viwili walizawadiwa Sh509,450 na Sh305,670, mtawalia.

Ni mara ya tano Mkenya ameshinda kitengo cha kinadada baada ya Caroline Kilel mwaka 2011, Mary Wacera (2015 na 2018) na Joan Chelimo (2017).

Kenya imerejesha taji la wanaume lililoenda Tanzania mwaka 2018. Kabla ya Gabriel Geay kutawala mwaka 2018, Kenya ilikuwa imeshinda kupitia kwa Geoffrey Mutai (2011 na 2012), Sambu (2013 na 2014), Daniel Salel (2015) na Chebii (2016 na 2017).

Makala ya mwaka huu yamevutia wakimbiaji 10, 000 kutoka mataifa 42 na kuchangisha Sh25,472,500.

You can share this post!

Migne atemwe asitemwe, mjadala wapamba moto baada ya kipigo

Puuzeni madai ya mpango wa kumuua Ruto – Wabunge

adminleo