Michezo

Wakenya walivyoduwaa Mtanzania akishinda taji la dunia la marathon Tokyo

Na GEOFFREY ANENE September 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KWA makala ya pili mfululizo Wakenya waliambulia pakavu katika mbio za kilomita 42 za wanaume kwenye Riadha za Dunia baada ya wawakilishi wake Kennedy Kimutai, Vincent Ngetich na Hillary Kipkoech kusikitisha mjini Tokyo nchini Japan, Jumanne alfajiri.

Katika siku ambayo Tanzania ilipata dhahabu ya kihistoria kupitia kwa Alphonce Simbu, Kimutai alikuwa Mkenya wa kwanza katika nafasi ya 16, Ngetich akakamata nafasi ya 22 naye Kipkoech akashindwa kumaliza mbio hizo.

Simbu alitwaa taji kwa saa 2:09:48 akifuatiwa na Mjerumani Amanal Petros (2:09:48) na Mwitaliano Iliass Aouani (2:09:53). Kimutai alikamilisha umbali huo kwa 2:11:45, Ngetich (2:13:38) naye Kipkoech aliishiwa pumzi kabla ya kufika utepeni.

Felix Simbu wa Tanzania apeperusha bendera ya taifa lake akisherehekea kushinda mbio hizo za marathon Jumanne. PICHA | REUTERS

Watimkaji 88 walianza mbio hizo, lakini 66 ndio walizikamilisha. Ethiopia, ambayo ilikuwa imenyakua medali ya 42km ya wanaume katika makala yote tangu 2009, iliambulia patupu Tesfaye Deriba, Deresa Geleta na Tadese Takele kujiuzulu.

Mkenya wa mwisho kushinda medali katika marathon ya wanaume kwenye Riadha za Dunia ni Amos Kipruto aliyepata shaba mwaka 2019 mjini Doha, Qatar.

Kenya haikupata medali katika makala ya 2022 mjini Eugene, Amerika na 2023 mjini Budapest, Hungary kabla ya ukame huo kuongeza Septemba 15, 2025.

Matokeo ya wanaume 42km (25-bora):

Alphonce Simbu (Tanzania) saa 2:09:48

Amanal Petros (Ujerumani) 2:09:48

Iliass Aouani (Italia) 2:09:53

Haimro Alame (Israel) 2:10:03

Abel Chelangat (Uganda) 2:10:11

Yohanes Chiappinelli (Italia) 2:10:15

Gashau Ayale (Israel) 2:10:27

Samsom Amare (Eritrea) 2:10:34

Clayton Young (Amerika) 2:10:43

Isaac Mpofu (Zimbabwe) 2:10:46

Ryota Kondo (Japan) 2:10:53

Cameron Levins (Canada) 2:11:07

Richard Ringer (Ujerumani) 2:11:14

Suldan Hassan (Uswidi) 2:11:18

Victor Kiplangat (Uganda) 2:11:33

Kennedy Kimutai (Kenya) 2:11:45

Koen Naert (Ubelgiji) 2:12:52

Abderrazak Charik (Algeria), 2:13:06

Kaan Kigen Ozbilen (Uturuki) 2:13:27

Mohamed Reda El Aaraby (Morocco) 2:13:29

Yaseen Abdalla (Sudan) 2:13:32

Vincent Ngetich (Kenya) 2:13:38

Naoki Koyama (Japan) 2:13:42

Peter Lynch (Ireland) 2:14:12

Ebba Chala (Uswidi) 2:14:40