Wakenya watatu kushiriki Dubai Marathon
Na GEOFFREY ANENE
WAKENYA Emmanuel Saina, Ruth Chepng’etich na Sharon Cherop wako katika orodha ya wakimbiaji 30, 000 wanaotarajiwa kutimka katika makala ya 20 ya mbio za Dubai Marathon katika Milki za Kiarabu, Ijumaa.
Saina alianza enzi yake ya marathon kwa kunyakua taji la Buenos Aires Marathon kwa saa 2:05:21 mwezi Septemba mwaka 2018. Atakuwa akishiriki mbio zake za pili za kilomita 42. Saina atapata ushindani mkali kutoka kwa wakimbiaji wa Ethiopia ambao wametawala kitengo cha wanaume cha Dubai Marathon tangu mwaka 2012.
Guye Adola, ambaye alibabaisha nyota Eliud Kipchoge katika Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2017 kabla ya kumaliza nyuma yake, ni mmoja wa wakimbiaji 14 kutoka Ethiopia ambao Saina atalazimika kutifulia vumbi kupata taji.
Naye malkia wa Istanbul Marathon, Chepng’etich atapambana na Cherop, ambaye anarejea Dubai baada ya kumaliza katika nafasi ya saba jijini humu mwaka 2012, pamoja na Waethiopia wanane akiwemo bingwa wa Dubai Marathon mwaka 2017 Worknesh Degefa.
Kwa miaka mingi, Dubai Marathon imevutia majina makubwa kwa kuwa marathon tajiri duniani ambayo ilishuhudia mshindi akitunukiwa Sh20.2 milioni. Mambo yamebadilika mwaka huu ambapo waandalizi wametangaza kwamba zawadi zimepunguzwa.
Mshindi sasa atapokea Sh10.1 milioni. Tuzo ya wakimbiaji wengine wote watakaomaliza ndani ya mduara wa 10-bora pia imepunguzwa kwa kukatwa katikati.
Mabadiliko haya ya zawadi yamechangiwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kuwacha Dubai Marathon nje ya orodha ya mbio za Platinum Label katika mbinu yake ya uorodheshaji wa riadha inayohitaji wakimbiaji 15, 000 kumaliza mbio ndiposa ijumuishwe katika kiwango hicho cha juu kabisa.