Michezo

Wakenya watatu, raia mmoja wa kigeni kuhojiwa zaidi katika mchakato wa kupata kocha mpya wa Shujaa

August 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

DALILI zote sasa zinaashiria kwamba kocha mpya wa timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, atakuwa mzaliwa wa humu nchini.

Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Raga katika Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), Thomas Odundo, kufichua kwamba raia mmoja wa kigeni na Wakenya watatu wamefaulu kuunga orodha fupi ya mwisho kabisa ya wakufunzi wanne watakaohojiwa kwa kina zaidi kufikia mwisho wa wiki hii.

“Orodha ya mwisho ina majina ya Wakenya watatu na kocha mmoja wa kigeni. Mahojiano ambayo yameendeshwa wiki mbili zilizopita sasa yanaelekea kukamilika. Maamuzi kuhusu nani atakayekuwa mkufunzi mpya wa Shujaa yatafanywa hivi karibuni na mshindi kutangazwa rasmi kufikia mwisho wa Agosti au mwanzoni mwa Septemba,” akasema Odundo.

Awali katika mahojiano yake na Taifa Leo, Ian Mugambi ambaye ni Katibu Mkuu wa KRU, alisema: “Tulikuwa na jumla ya makocha 15 waliotuma maombi ya kazi. Kati ya hao, watatu ni Wakenya na 12 walikuwa raia wa kigeni hasa kutoka New Zealand, Australia, Afrika Kusini na Uingereza. Tulifanya mchujo na kusalia na orodha fupi ya wawaniaji sita kisha wanne.”

Mmoja kati ya wanne hao kwenye orodha fupi ya mwisho atapata nafasi ya kurithi mikoba iliyoachwa na Paul Feeney – kocha raia wa New Zealand aliyeagana rasmi na KRU mnamo Juni 12, 2020.

“Jina la atakayeteuliwa mwishowe na Jopo la Mahojiano litawasilishwa kwa Bodi ya KRU kabla ya kocha huyo kutambulishwa rasmi kwa kikosi na mashabiki,” akaongeza Mugambi.

Kwa mujibu wa wadokezi mbalimbali wa shirikisho waliotaka majina yao yabanwe, huenda Bodi ya KRU ikawa radhi zaidi kumpa kocha wa humu nchini fursa ya kudhibiti mikoba ya Shujaa hasa ikizingatiwa hali ngumu ya kiuchumi ambayo imechangiwa na mkurupuko wa virusi vya corona.

“KRU haitakuwa tayari kumwajiri kocha wa kigeni atakayetaka kudumishwa kwa mshahara mkubwa wakati huu ambapo corona imelemaza hazina ya mashirikisho mbalimbali ya michezo,” akasema mmoja wa wadokezi wetu.

KRU inasaka mkufunzi atakayeongoza Shujaa kwenye Michezo ya Olimpiki ambayo imeahirishwa hadi mwaka ujao jijini Tokyo, Japan.

Kibarua cha kwanza cha kocha huyo mpya, ambaye atakuwa wa 10 kudhibiti mikoba ya Shujaa chini ya kipindi cha miaka tisa iliyopita, kitakuwa ni kuongoza Kenya kuwa mwenyeji wa kipute cha kimataifa cha Safari Sevens.

Baadhi ya wakufunzi ambao wamenoa Shujaa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ni Mitch Ocholla (2011-12), Mike Friday wa Amerika (2012-13), Paul Treu wa Afrika Kusini (2014), Felix ‘Toti’ Ochieng (2015), Benjamin Ayimba (2016-17), Innocent ‘Namcos’ Simiyu (2018) na Paul Murunga (2019).

Chini ya Feeney, Shujaa walifuzu kwa makala yajayo ya 32 ya Michezo ya Olimpiki na kukamilisha kampeni za Raga ya Dunia muhula huu wa 2019-20 katika nafasi ya 12 kwenye orodha ya timu 15. Kenya ilijizolea jumla ya alama 35 na kutinga robo-fainali za Main Cup mara mbili jijini Cape Town (Afrika Kusini) na Hamilton (New Zealand).

Feeney, ambaye pia aliongoza Kenya Morans kutinga fainali ya Tusker Safari Sevens mwaka 2019, aliteuliwa kuwa kocha wa Shujaa mnamo Septemba 2019 baada ya mkataba wa Murunga kutamatika.

Amewahi pia kunoa timu ya taifa ya Fiji na vikosi vya raga vya Auckland na Stormers nchini New Zealand na Afrika Kusini mtawalia.