Michezo

Wakenya watawala Taipei Marathon

March 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

WAKIMBIAJI Mathew Kipsaat na Naomi Jepkogei Maiyo kutoka Kenya walitia mfukoni Sh1,006,100 kila mmoja kwa kuibuka washindi katika mbio za New Taipei City Wan Jin Shi Marathon hapo Machi 17, 2019.

Kipsaat na Maiyo waliongezwa Sh503,150 kwa kuweka rekodi mpya za New Taipei City Wan Jin Shi ambazo ni saa 2:11:17 na 2:34:08, mtawalia.

Kipsaat alikuwa katika kundi la kwanza la wakimbiaji wanne hadi kilomita ya 29 pale alipoongeza kasi na kuvunja rekodi ya saa 2:13:05 ambayo Mkenya William Chebon Chebor aliweka mwaka 2016.

Alikimbia vyema akifungua mwanya wa sekunde 18 alipofika kilomita ya 30 na kuiongeza hadi zaidi ya dakika moja katika kilomita ya 35 na kufungua mwanya wa zaidi ya dakika mbili alipofika kilomita ya 40.

Kipsaat alifuatwa na Wakenya wenzake Philip Cheruiyot Kangogo (2:13:57) na Alex Chepkwik Saekwo (2:15:18).

Maiyo alikuwa katika kundi la kwanza la watu watano kabla ya kujitosa mbele baada ya kilomita ya 35.

Alifungua mwanya wa sekunde 38 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Meseret Sisay alipofika kilomita ya 40 kabla ya kukata utepe akiimarisha muda wake bora kwa sekunde 45.

Muethiopia Sisay alimaliza katika nafasi ya pili (2:34:51), huku Mkenya Ednah Mukhwana akiridhika katika nafasi ya tatu (2:35:01).