Wakufunzi wapya wa Kabras RFC kutua nchini Jumamosi
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA mpya wa Kabras RFC, Mzingaye Nyathi na msaidizi wake Felix Reyon wanatarajiwa kutua humu nchini mnamo Jumamosi kutoka Zimbabwe na Afrika Kusini mtawalia.
Wawili hao waliteuliwa kudhibiti mikoba ya Kabras mnamo Julai na Agosti mtawalia kwa mkataba wa miaka mitatu kila mmoja. Wanatazamiwa kutambulishwa rasmi kwa kikosi na mashabiki wiki ijayo kabla ya kusuka njama ya kutamalaki kampeni za msimu ujao wa 2020-21 katika kivumbi cha Kenya Cup na mapambano mengine ya raga ya humu nchini.
Mwenyekiti Phillip Jalango amesema mikutano ya kubuni mikakati kabambe ya kuboresha uthabiti wa kikosi itaandaliwa na wakufunzi hao wawili huku wakisubiri mwelekeo utakaotolewa na Wizara ya Michezo kuhusu jinsi ya kurejelewa kwa spoti katika kipindi hiki cha corona.
“Tunataka kuweka msingi imara na kuanza kujipanga kwa minajili ya msimu mpya. Tunahitaji kusuka kikosi kizuri na kuwapa makocha wapya fursa ya kujifahamisha na wachezaji na maafisa wengine wa benchi ya kiufundi,” akasema Jalango.
Mwanaraga wa zamani wa Kenya Simbas, Edwin Achayo atadhibiti sasa mikoba ya chipukizi wa Kabras akisaidiana na Richard Ochieng ambaye kwa sasa ni kocha wa viungo. Jerome Paarwater ambaye ni kocha wa zamani wa Simbas ndiye Mkurugenzi wa Raga wa Kabras.
Jalango aliongeza kwamba wanaraga wa Kabras wamekuwa wakijifanyia mazoezi kwa miezi kadhaa iliyopita. Kinara huyo ni mwingi wa matumaini kwamba watahimili ushindani mkali wanaotarajia msimu ujao kwa kuwa wamefaulu kudumisha wachezaji wao tegemeo.
“Idadi kubwa ya wanaraga tuliowategemea msimu uliopita wamesalia kikosini na kiu ya kutamalaki vipute mbalimbali ingalipo. Tunatarajia kujivunia matokeo ya kuridhisha hata zaidi kuliko muhula uliopita,” akaongeza Jalango.
Miongoni mwa wanaraga mahiri watakaoendelea kutegemewa na wanasukari wa Kabras ni George Nyambua, Dan Sikuta, Asman Mugerwa, Hillary Odhiambo, Max Adaka, Brian Tanga, Felix Ayange na Nick Barasa.
Baada ya kuteuliwa mwezi uliopita, Nyathi alisema kubwa zaidi katika maazimio yake ni kurejesha uthabiti uliowawezesha Kabras kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya Cup mnamo 2016 na ufalme wa Enterprise Cup mnamo 2019.
Kabras wamezidiwa maarifa na wanabenki wa KCB katika fainali tatu zilizopita za Kenya Cup, rekodi mbovu ambayo Nyathi atapania kutamatisha.
Hadi kusitishwa kwa raga ya humu nchini mnamo Machi kutokana na janga la corona, Kabras walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 74 chini ya ukufunzi wa Henley Plessis wa Afrika Kusini. Kabras walitarajiwa kuvaana na mshindi kati ya Impala Saracens na Mwamba RFC katika hatua ya nusu-fainali.
Mbali na kudhibiti mikoba ya Uitenhage nchini Afrika Kusini kati ya 2006 na 2009, Reyon, 49, amewahi pia kunoa kikosi cha Port Elizabeth Harlequins mnamo 2005 kisha katika msimu wa 2019-20 na kikosi cha Eastern Province katika Currie Cup (2009) na Vodacom Cup (2010).
Kwa upande wake, Nyathi, 45, amewahi kutia makali vikosi vingi vya Afrika Kusini vikiwemo Camps Bay na Western Province. Katika enzi zake za uchezaji, aliwahi kuvalia jezi za timu ya taifa ya Zimbabwe Sables na klabu za Old Miltonians na Old Hararians jijini Bulawayo.