Walcott aahidi makuu baada ya kufungia Southampton katika sare ya 1-1 dhidi ya Wolves ugenini
Na MASHIRIKA
FOWADI Theo Walcott amesema kwamba anajihisi “mtoto kwa mara nyingine” baada ya kufunga bao la kwanza tangu ajiunge upya na Southampton katika sare ya 1-1 waliyoisajili dhidi ya Wolves kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Novemba 23, 2020.
Walcott, 31, alirejea kambini mwa Southampton kwa mkopo wa msimu mmoja zaidi kutoka Everton mnamo Oktoba 2020. Aliwahi kuwa mchezaji wa kikosi hicho hadi alipotua Arsenal mnamo 2006 akiwa na umri wa miaka 16 pekee.
Chini ya kocha Ralph Hasenhuttl, Walcott ambaye ni raia wa Uingereza, aliwaweka Southampton kifua mbele kunako dakika ya 58 ugani Molineux baada ya kukamilisha kwa ustadi krosi ya Che Adams.
Ingawa hivyo, bao hilo halikutosha kuwavunia Southampton alama tatu muhimu walizozihitaji ili kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa kuwa Pedro Neto alisawazisha mambo katika dakika ya 75 baada ya kushirikiana vilivyo na fowadi raia wa Mexico, Raul Jiminez.
Sare iliyosajiliwa na Southampton dhidi ya Wolves iliwasaza katika nafasi ya tano jedwalini kwa alama 17, tatu nyuma ya viongozi Tottenham Hotspur na mabingwa watetezi, Liverpool.
“Nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kuongoza Southampton kushinda michuano mingi iwezekanavyo. Kocha ana imani kubwa kwangu na matarajio kutoka kwa mashabiki ni ya kiwango cha hali ya juu. Nakithamini sana kikosi hiki na nina kila sababu ya kukistahi kwa kunipokeza malezi ya awali kabisa katika soka,” akatanguliza Walcott.
“Kuvalia jezi za Southampton kunanifanya kujihisi mtoto mdogo na ninaamini bao nililowafungia litanichochea zaidi kufanya makuu kwa sababu ningali na mengi ya kufanikisha katika ulingo wa soka ya Uingereza,” akaongeza.
Southampton kwa sasa hawajapigwa katika mchuano wowote kati ya saba iliyopita na walipoteza nafasi nyingi za kufanya mambo kuwa 2-0 katika kipindi cha pili.
Kwa upande wao, Wolves walipaa hadi nafasi ya tisa kwa alama 14 sawa na West Ham United ya kocha wa zamani wa Manchester United, David Moyes. Wolves wamepoteza mchuano mmoja pekee kati ya saba iliyopita kwenye EPL katika uwanja wao wa nyumbani wa Molineux.
Kikosi hicho kwa sasa kinajiandaa kuvaana na Arsenal ugani Emirates mnamo Novemba 29 huku Southampton wakiwaalika Manchester United siku hiyo uwanjani St Mary’s.