Michezo

Wanabondia Fury na Joshua kunogesha mapigano yao jijini London mnamo Disemba 2020

October 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

BONDIA Tyson Fury ambaye ni mshikilizi wa taji la WBC la uzani wa ‘heavy’ atashiriki ndondi za haiba kubwa jijini London, Uingereza mnamo Disemba 5, 2020 dhidi ya mshindani ambaye atafichuliwa “hivi karibuni”.

Frank Warren ambaye ni promota wa Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 32 amesema kwamba Fury amefutilia mbali mpango wa kuchapana na Deontay Wilder wa Amerika kwa mara ya tatu mnamo Disemba 2020 na tayari amepata mshindani mpya.

Fury alimdengua Wilder kwa njia ya ‘Knock-Out’ katika raundi ya saba ya masumbwi yaliyoandaliwa jijini Las Vegas, Amerika mnamo Februari 2020. Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Fury kumzidi maarifa Wilder baada ya wawili hao kuambulia sare mnamo 2018 jijini Los Angeles, Amerika.

“Natamani sana kurejea ulingoni kuendelea kufanya kitu ninachokifahamu vyema zaidi,” akasema Fury.

Kwingineko, mwanamasumbwi Anthony Joshua amethibitisha kwamba atashuka dimbani kutetea mataji yake ya kimataifa ya IBF, WBA, WBO na IBO katika uzani wa ‘heavy’ kwenye pigano litakalomkutanisha na Kubrat Pulev wa Bulgaria mnamo Disemba 12 kwenye ukumbi wa The O2 jijini London.

Wawili hao walikuwa wameratibiwa kuchapana makonde katika uwanja wa Tottenham Hotspur jijini London, Uingereza mnamo Juni 20, 2020 kabla ya mchapano huo kuahirishwa.

Kwa mujibu wa Matchroom Boxing ambao ni mapromota wa Joshua, yalikuwa matamanio yao kufanikisha pigano hilo uwanjani ugani Tottenham.

Joshua, 30, hajashiriki ndondi zozote tangu Disemba 2019 baada ya kumzidi maarifa Andy Ruiz Jr kwa wingi wa alama nchini Saudi Arabia. Mchapano huo ulimpa Joshua jukwaa maridhawa la kurejesha ufalme aliokuwa amepokonywa hapo awali na mwanamasumbwi huyo mzawa wa Amerika na raia wa Mexico jijini New York, Amerika mnamo Juni 2019.

Pulev, 38, atakuwa akiwania fursa ya kutwaa taji la IBF kutoka kwa Joshua. Awali, wawili hao walikuwa wamepangwa kumenyana mnamo Oktoba 2019 uwanjani Cardiff Principality, Uingereza. Hata hivyo, Pulev alijiondoa katika dakika za mwisho baada ya kupata jeraha baya la bega.

Michuano yote iliyokuwa imeratibiwa na Bodi ya Ndondi ya Uingereza hadi mwisho wa Mei 2020 ilifutiliwa mbali kutokana na virusi vya corona vinavyozidi kutikisa ulimwengu mzima na kuvuruga kalenda ya michezo mbalimbali.

Eddie Hearn ambaye ni promota wa Pulev amesema bondia wake yuko ange kwa pigano hilo.

Kwa upande wake, Fury amesema: “Nawahakikishia mashabiki wangu kwamba nitakuwa ulingoni mnamo Disemba 5 jijini London. Mpinzani wangu atajulikana chini ya kipindi cha wiki moja ijayo. Tarajieni mambo makubwa.”

Fury hajawahi kushiriki mashindano yoyote nchini Uingereza tangu Agosti 2018. Mashindano yake manne yaliyopita yaliandaliwa nchini Amerika.

“Pigano langu dhidi ya Wilder lilikuwa awali lifanyike Julai 2020 kabla ya kuahirishwa hadi Oktoba kisha Disemba 19. Sasa waandalizi wamezungumzia uwezekano wa pambao hilo kufanyika mwaka ujao wa 2021 japo nimechoka sana kusubiri na huenda nikateua kususia,” akasema Fury.