Michezo

Wanabunduki roho juu wakiendea ‘mboga’ EPL Jumatatu usiku

March 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

ARSENAL watashuka leo ugani Bramall Lane wakipigiwa upatu wa kukomoa Sheffield United na kuendeleza presha kwa Liverpool na mabingwa watetezi Manchester City kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Idadi kubwa ya mabao (10) ambayo Sheffield United wamefungwa katika mechi mbili kati ya nne zilizopita ligini imewasaza katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za muhula huu.

Sasa wanavuta mkia kwa alama 13 pekee kutokana na mechi 26 huku Arsenal wakikamata nafasi ya tatu kwa pointi 58. Pengo la alama tano linatamalaki kati ya Arsenal na viongozi wa jedwali Liverpool waliotandika Nottingham Forest 1-0 ugani City Ground, Jumamosi.

Tofauti na Sheffield United waliokubali kichapo cha 1-0 kutoka kwa Wolverhampton Wanderers katika pambano lao lililopita la EPL, Arsenal watajibwaga ulingoni wakipania kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 4-1 dhidi ya Newcastle United uwanjani Emirates.

Japo Sheffield United hawajawahi kupoteza mchuano wowote wa ugenini kwa zaidi ya bao moja mwaka huu wa 2024, kikosi hicho kimekuwa kikisuasua pakubwa nyumbani.

Aston Villa waliwakomoa 5-0 katika EPL mnamo Februari 3 kabla ya Brighton waliowanyoa 5-2 katika raundi ya Kombe la FA mwishoni mwa Januari kuwakung’uta tena 5-0 ligini mnamo Februari 18.

Iwapo Arsenal itawafunga angalau mabao matano hii leo, basi wataweka rekodi duni ya kuwa kikosi cha kwanza katika EPL kuwahi kupoteza mechi tatu mfululizo kwa idadi hiyo ya magoli.

Aidha, itakuwa timu ya kwanza kuwahi kupoteza michuano minne mfululizo ya mashindano yote kwa mabao matano katika uwanja wao wa nyumbani.

Huku Sheffield United wakitawaliwa na kiu ya kukwepa rekodi hiyo duni, Arsenal kwa upande wao wana ari ya kuendelea kubebesha wapinzani wao idadi kubwa ya mabao katika kampeni za EPL.

Hadi walipopepeta Newcastle 4-1, vijana hao wa kocha Mikel Arteta walikuwa wameponda West Ham United 6-0 kabla ya kucharaza Burnley 5-0 katika michuano miwili iliyopita ya EPL ugenini.

Ushindi kwa Arsenal leo utakuwa wao wa saba mfululizo katika EPL na wa nne dhidi ya Sheffield United. Miamba hao wanafukuzia taji la kwanza la EPL tangu msimu wa 2003-04, walipepeta Sheffield United 5-0 katika mkondo wa kwanza wa EPL ugani Emirates mnamo Oktoba 2023.

Mechi mbili zilizopita ambazo wametandaza ugani Bramall Lane zimewashuhudia wakishinda 2-1 katika robo-fainali ya Kombe la FA mnamo 2019-20 kabla ya kuibuka na ushindi wa 3-0 katika EPL mnamo Aprili 2021.

Tofauti na Sheffield United wanaokabiliwa na visa vingi vya majeraha, Arsenal watakuwa bila Oleksandr Zinchenko, Takehiro Tomiyasu na Jurrien Timber wanaoendelea kupona. Gabriel Jesus na Thomas Partey wanatarajiwa kurejea katika kikosi cha kwanza.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):
Brentford 2-2 Chelsea
Everton 1-3 West Ham
Fulham 3-0 Brighton
Newcastle 3-0 Wolves
Nottm Forest 0-1 Liverpool
Tottenham 3-1 Palace
Luton Town 2-3 Aston Villa