Wanafunziwa LGS watamba mashindano ya mpira wa vikapu
WANAFUNZI kutoka Light Group of Schools (LGS) walionyesha talanta ya juu katika mashindano ya mpira wa vikapu yaliyoandaliwa Shule ya Kimataifa ya Crawford.
Ilikuwa dhahiri kuwa kipaji chao kikipaliliwa, basi huenda wakaibuka na kuwa wachezaji mahiri wa vikapu na hata kusaidia timu ya taifa kung’aa katika mashindano mbalimbali miaka inayokuja.
Mashindano hayo yalishirikisha shule saba na wanafunzi hao walionyesha ukwasi wa talanta huku wakiwapiku washindani wao .
“Huwa hatuwaandai wanafunzi kwa ajili ya mtihani pekee bali pia kuhakikisha kuwa tunakuza talanta zao kupitia michezo mbalimbali na hata mchezo wa kuigiza,” akasema Mwalimu wa LGS Felix Ochieng’.
Hasa alisema wamekuwa wakijikita kwenye mpira wa vikapu kwa sababu unawasaidia wanafunzi kuwa na maadili, nidhamu na pia kuwashirikisha kwenye mafunzo ya uongozi ili wawe viongozi bora siku zijazo.
“Michezo ni sehemu muhimu ya safari ya wanafunzi katika shule ya LGS, na tunajivunia kuunga mkono ndoto zao katika nyanja mbalimbali,” akaongeza.
Kikosi cha wanafunzi wa kike kwenye mpira wa vikapu walivutia ushabiki hata kutoka kwa shule pinzani kutokana na jinsi walivyowalemea washindani wao.