Michezo

Wanakarate wa Kenya wazoa medali 39 India

March 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

TIMU ya karate ya Kenya ilizoa medali 39 katika mashindano ya karate ya ulimwengu yafahamikayo kama Asian International World Funakoshi Shotokan Karate Organisation (WFSKO) yaliyofanyika Jumapili mjini Mumbai, India.

Kocha wa kikosi hicho Elizabeth Rukwaro anasema aliongoza wanakarate wapatao 32 ambao ni wenye umri kati ya miaka minne na 17 kutoka Kaunti ya Kiambu na ile ya Murang’a.

Alisema mashindano hayo yalifanyika katika ukumbi wa Priyadarshini Indira Gandhi Sports Complex katika mji wa Mumbai, India.

Alisema katika kikosi alichoandamana nacho, 22 walitoka Kaunti ya Murang’ a, halafu 10 walitoka  Kiambu.

“Huu ni ushindi mkubwa kwa nchi ya Kenya. Kile tunachohitaji kama timu ni vifaa maalumu vya kuchezea. Iwapo Kaunti zetu mbili zitajizatiti na kununulia vijana hawa vifaa vyote vinavyohitajika, bila shaka mambo yatakuwa mazuri kwa kikosi chetu,” asema kocha Rukwaro.

Alitaja nchi zilizoshiriki mashindano hayo kama Sri Lanka, Kyrgyatan, Malaysia, Nepal, Iran, Uingereza, Armenia, Mauritius, Bhutan, na Kenya.

Alisema nchi ya Kenya imefuzu kucheza kwenye mashindano ya ulimwengu ya Karate yatakayofanyika Uingereza mnamo Novemba 2019.

“Mimi kwa sasa nitaendelea kufanya maandalizi kabambe ili niwe na vijana walioiva sawasawa,” alisema Rukwaro ambaye ndiye kocha wa pekee wa kike katika mchezo huo.

Anasema cha muhimu sasa ni kuona ya kwamba anapata kupewa sapoti inayostahili hata na wafadhili kutoka nje.

“Hii ni kazi inayostahili ushirikiano mkubwa ili kuifanikisha vilivyo. Kwa hivyo, ninaomba ushirikiano wa kila mmoja. Wazazi wa vijana hawa wameridhika na kazi njema ninayofanya kwa wanakarate hao,” alisema Rukwaro.

Alisema mazoezi yake anayaongoza katika shule ya msingi ya Makongeni, Thika na anawahimiza wazazi kuwapa watoto wao nafasi ya kuhudhuria mazoezi.