Michezo

Wanamichezo na skendo zao

Na MWANDISHI WETU April 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ISHU ya kipa Patrick Matasi bado haijapoa. Skendo yake ya upangaji mechi bado ipo midomoni mwa watu licha ya mahakama kupindua uamuzi wa FKF kumfungia kucheza soka kwa siku 30.

Wachanganuzi wengi wanasisitiza kuwa Matasi kwa skendo hiyo, alishajikoroga na kujiwesti vibaya kwani itakua ngumu yeye kupata timu tena.

Wengi wanasema huo ndio mwisho wa taaluma yake.

Lakini Matasi sio mwanamichezo wa kwanza kuwa na taaluma ya kufana kabla ya kujipiga bao.

Wapo mastaa hawa pia walioshindwa kumudu ustaa wao na mwisho wa siku wakaishia pabaya.

DANIEL ADONGO (Raga)

Adongo aliiteka tasnia ya raga humu nchini 2013 alipoibukia kuwa moja kati ya wachezaji matata katika timu ya taifa ya raga 15, Simba.

Hii ilikuwa ni baada yake kuonyesha kiwango sana kwenye mechi za kufuzu kushiriki dimba la dunia la raga 15, 2015.

Haikukawia kabla ya klabu ya Southern Kings ya kule Afrika Kusini kumsajili.

Barani Afrika, Sauzi inafahamika kuwa na ligi kuu bora zaidi ya raga 15s ifahamikayo kama Super Rugby.

Duniani Super Rugby inaorodheshwa ya pili kwenye ubora.

Huko Sauzi Adongo aliendelea kutamba na haikukawia kabla ya kupata mchongo Amerika.

Hata hivyo, alipofika kule, aliamua kuhamia American Football ambayo inashabihiana zaidi na raga.

Ghafla akawa staa mkubwa wa mchezo huo na mpenzi wa mashabiki.

Baada ya kung’aa na Indiana Colts iliyokuwa ikimfanyia majaribio, klabu hiyo iliamua kumzawadi na mkataba mnene uliokuwa ukimlipa Sh2.9 milioni kila mwezi.

Hata hivyo, baada ya kuichezea Colts mechi kadhaa, mkataba wake ulivunjwa na klabu hiyo Desemba 17, 2015 baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba Adongo alikuwa akimtandika na kumnyanyasa demu wake wa wakati huo.

Mara mbili demu huyo aliripoti kupigwa na Adongo.

Ni baada ya kuvunjiwa mkataba ndio maisha ya Adongo yakabadilika.

Anaripotiwa kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya, pamoja na imani za kishirikina.

Pesa zimekwisha na kwa sasa kageuka chokora katika mitaa huko Amerika.

CONJESTINA ACHIENG (Ndondi)

Ni bondia aliyeibeba sana taifa hili hilo hakuna anayeweza kupinga.

Enzi za upiganaji wake, Conjestina alimfanya kila mtu kuwa shabiki wa ngumi humu nchini.

Ngumi zake zilikuwa hatari na akaishia kupachikwa jina la utani ‘Hands of Stone’.

Licha ya kuiwakilisha taifa vizuri na kushiriki mashindano kadhaa zilizomlipa pesa za maana, Conje hakuweza kujiwekea akiba.

Alipostaafu ngumi baada ya miaka kumi, alianza kuugua sonona alipojikuta hana pesa.

Wale marafiki wa enzi za umaarufu wake wakamtoka. Mpaka leo Conje hajawahi kuwa sawa, bado anaendelea kuhangaika.

Wadau mbalimbali wamejaribu kumpa usaidizi wa matibabu lakini hali yake bado tete.

SAMUEL WANJIRU (Riadha)

Marehemu Wanjiru anakumbukwa kuwa mwanariadha wa kwanza wa Marathon kuwahi kuishindia Kenya nishani ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki.

Taaluma yake ilifana sana katika kipindi chote cha uhai wake na ndani ya miaka michache tu.

Wanjiru alijigeuza tajiri mkubwa kutokana na mamilioni ya fedha alizokuwa akilipwa baada ya kushinda mashindano.

Hadi alipofariki dunia akiwa na miaka 25 tu, utajiri wake ulikuwa ni zaidi ya Sh200 milioni.

Tatizo la Wanjiru ni kwamba alishindwa kabisa kumudu nidhamu yake.

Pesa zilimpa ujeuri, ustaa ukampa kiburi. Alipenda wanawake na pombe.

Hata wakati wa kifo chake, alikuwa kwenye mgogoro na wanawake. Wanjiru anadaiwa kufumaniwa na mke wake Teresa Njeri nyumbani kwao Nyahururu akiwa na mwanamke mwingine chumbani.

Anasemekana alikuwa amelewa. Alikumbana na mauti yake alipoanguka kutoka kwenye ghorofa lake akijaribu kuruka ukuta kwenda kumzuia mke wake Teresa asiondoke.

Ripoti za polisi ziliarifu kuwa Wanjiru alikuwa mlevi wakati wa kifo chake.

MAURICE ODUMBE (Kriketi)

Kuna miaka ambayo Kenya ilitamba sana katika mchezo huu wa Kriketi.

Ni enzi ambazo ilikuwa na wachezaji nyota kama Maurice Odumbe.

Licha ya kuwa na fursa nzuri ya kunawari kama mchezaji na kuweza kusaka ulaji kwingine, Odumbe aliamua kuwa muhuni.

Aliamua kutumia umaarufu wake miaka hiyo kucheza dili chafu chafu za kupanga matokeo za mechi.

Mwaka 2004 Kamati ya Kimataifa ya Kriketi ilimpiga marufuku ya miaka minne baada ya kumpata na hatia ya kuhusika kwenye upangaji matokeo.

Kamati hiyo ilibaini kuwa Odumbe alikuwa amelipwa fedha ili afixi mechi. Marufuku hiyo ikamaliza taaluma ya kufana ya Odumbe.

Ustaa na umaarufu ukapotea. Mkwanja ukaisha. Odumbe akaanza kuugua na toka kipindi hicho mpaka leo, anaishi kwenda ‘rehab’ akitoka na kurudi.

ASBEL KIPROP (Riadha)

Kwa miaka kumi Kiprop alitawala mbio za mita 1,500 akiibuka bingwa wa dunia mara tatu.

Hata hivyo, Kiprop aliiacha taifa hoi 2017 alipopatikana na makosa ya pufya.

Athletics Intergrity Unit ilimpata na makosa ya kutumia EPO moja ya dawa za kusisimua misuli zilizoharamishwa. Akafungiwa riadha kwa miaka minne jambo lililovuruga akili. Akaanza kuugua sonona.

Akageukia pombe. Akaanza kuchepuka na kumfanya mke wake kumtoroka. Kuna wakati alishtua dunia, alipodai kwamba kama hatapokonywa bunduki yake ya kazi basi ataitumia kujiua.

Posti hiyo kwenye Facebook ilimpelekea Inspekta Jenerali wa Polisi wakati huo Hilary Mutyambai kuingilia kati kumsaidia. Ila huo ukawa ndio mwisho wa ustaa wake.