Wanariadha sasa wageuka kuwa wafugaji mahiri
Na CHRIS ADUNGO
TANGU Machi 13, 2020 ambapo kisa cha kwanza cha virusi vya corona kilipothibitishwa humu nchini, shughuli zote za michezo zilisitishwa na Serikali.
Kati ya walioathiriwa vikali na hatua hiyo ni wanariadha ambao kwa sasa wameanza kujishughulisha na masuala mengineyo yakiwemo kilimo na ufugaji baada ya kambi zao za mazoezi kufungwa.
Beatrice Chepkoech ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji sasa hutumia mwingi wa muda wake kusaidia wazazi wake kuchuma majani-chai na kutafuta kuni katika kijiji cha Besiobei, eneo la Konoin, Kaunti ya Bomet.
“Msimu wote unaelekea sasa kupotea na nimesalia kujifanyia mazoezi mepesi baada ya kufanya kazi chache za shambani pamoja na wazazi wangu,” akasema Chepkoech ambaye ameapa kuvunja rekodi yake mwenyewe na kutwaa medali ya dhahabu katika Olimpiki za mwaka ujao jijini Tokyo, Japan.
Kwa upande wake, Rodgers Kwemoi naye anajishughulisha na kilimo cha mahindi ambayo kwa sasa anayapalilia katika kijiji cha Furfural, eneo la Matunda, Kaunti ya Uasin Gishu.
Kwemoi aliibuka bingwa wa dunia katika mbio za mita 10,000 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2016.
“Kwa sasa napalilia mahindi na kunyunyizia dawa za kuua wadudu. Tumeathiriwa pakubwa na janga hili ambalo limetuacha tukikadiria hasara tupu,” akasema Kwemoi ambaye hukimbilia kikosi kimoja nchini Japan.
Kauli ya Kwemoi ilishadidiwa na bingwa mwingine wa dunia katika mbio za mita 10,000 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Rhonex Kipruto ambaye kwa sasa anapanda miche ya miti mbalimbali katika kijiji cha Kimamet, eneo la Kamwosor, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Bingwa wa mbio za New York City Marathon, Joyciline Jepkosgei, amesema kuahirishwa kwa marathon za London na Ney York City zilizokuwa zifanyike Aprili na Novemba 2020 mtawalia, ni kati ya matukio ambayo yamemvunja moyo katika ulingo wa riadha.
Jepkosgei anashikilia kwamba alikuwa amejiandaa vilivyo kwa mbio hizo ambazo kuahirishwa kwazo kumemtia katika ulazima wa kukadiria hasara kubwa.
“Sawa na mwanariadha yeyote, nilijihisi vibaya sana baada ya kivumbi cha London Marathon kufutiliwa mbali. Nilikuwa na uhakika wa kuzitawala mbio hizo na hatimaye kutwaa nishani ya dhahabu,” akatanguliza.
“Nilikuwa nimejiandaa vya kutosha na kuwekeza kiasi kikubwa cha raslimali mazoeini. Ingawa hivyo, imenibidi kukubali matokeo na maamuzi hayo japo bado nahisi kuvunjika moyo kabisa,” akasema mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia katika mbio za Nusu Marathon.
Ili kukabiliana na msongo wa mawazo, mshindi huyo wa zamani wa medali ya shaba katika mbio za mita 10,000 barani Afrika, amesema kuwa kwa sasa amepania kujishughulisha na masuala ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kilimo cha viazi katika eneo la Iten, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet.
Jepkosgei aliyeibuka mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za Ras Al Khaimah (RAK) mnamo 2017, amekuwa pia akishiriki mazoezi mepesi ili kudumisha ubora wa fomu yake sawa na anavyofanya bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500, Elijah Manangoi, 27.
Manangoi ambaye kwa sasa anajishughulisha na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo katika eneo la Narok alijizolea nishani ya fedha katika mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia mnamo 2015 jijini Beijing, China kabla ya kutwaa dhahabu katika mbio hizo miaka miwili baadaye jijini London, Uingereza.
Jeraha ambalo limemweka nje kwa muda mrefu lilikuwa kiini cha kukosekana kwake katika Riadha za Dunia zilizoandaliwa mwaka jana jijini Doha, Qatar. Huu ulikuwa msimu wa Manangoi kurejea katika ulingo wa riadha kwa matao ya juu na alikuwa akipania kutawala duru zote za mbio za Diamond League.