Wanariadha wamwomboleza Ben Jipcho
Na CHRIS ADUNGO
ULINGO wa riadha umepoteza mwanariadha stadi Ben Jipcho ambaye aliaga dunia hapo jana katika hospitali ya Fountain mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu alikokuwa amelazwa kwa kipindi cha siku tatu.
Jipcho ni mshindi wa zamani wa nishani ya fedha katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Olimpiki za 1972.
Kwa mujibu wa mwanawe wa kike, Ruth Jipcho, nguli huyo wa riadha alifariki saa tisa alfajiri akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
“Baba yetu aliugua kwa muda. Hatimaye Mola alimpumzisha usiku wa kuamkia Ijumaa ya Julai 24, 2020. Amekuwa akitatizwa sana na maradhi ya mapafu, figo na ini,” akasema Ruth.
Wiki iliyopita, Jipcho alipata maradhi ya tumbo na akapelekwa katika Hospitali ya Crystal mjini Kitale alikotibiwa na kushauriwa kutafuta matibabu zaidi mjini Eldoret kabla ya hali yake ya afya kudorora.
Akimwomboleza Jipcho, Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (Nock), Paul Tergat, alisema kwamba Jipcho ndiye baba mwanzilishi wa riadha za Kenya ambaye aliwafungulia watimkaji wote wazawa wa humu nchini milango ya heri na hatimaye kutamba katika ulingo wa kimataifa.
“Kifo kimetupiga pute johari adimu na kito cha thamani katika ulingo wa riadha. Tumesikitishwa sana na kifo cha Jipcho ambacho tumepokea kwa mshtuko mkubwa. Mola aifariji familia na wote walioguswa na kuondoka kwake,” akasema Tergat.
Mwingine ambaye aliongoza Wakenya kumwomboleza Jipcho ni aliyekuwa Mbunge wa Cherangany na bingwa wa Boston Marathon 2012, Wesley Kipchumba Korir.
Korir alisema kuwa alimjua Jipcho kama mwanariadhaa mkomavu wa enzi zake ambapo aliletea nchi hii sifa tele yakiwemo mataji ya haiba.
“Ni miongoni mwa watimkaji ambao waliwawekea wanariadhaa chipukizi msingi wa kushindana katika majukwaa ya kimataifa, mimi nikiwamo. Familia ya wanariadha imempoteza mtu mashauri ambaye atakumbukwa kwa kukuza talanta za wanariadha wengi humu nchini. Alitegemewa sana kwa mawaidha na ni muhali sana kujaza pengo ambalo ameliacha,” akasema.
Jipcho alijitosa rasmi katika ulingo wa riadha katika miaka ya 60 na anakumbukwa kwa kujinyima nafasi ya kutwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 alizomwachia Mkenya mwenzake Kipchoge Keino kwenye Olimpiki za 1968 nchini Mexico.
Mnamo 1970, Jipcho alijizolea nishani ya fedha katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Edinburgh, Scotland kabla ya kuambulia tena nafasi ya pili katika mbio hizo kwenye Olimpiki za 1972 jijini Munich, Ujerumani.
Mnamo 1973, alizoa medali za dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Michezo ya Bara la Afrika iliyoandaliwa jijini Lagos, Nigeria.
Mnamo 1974, Jipcho alitwaa nishani za dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji kisha akaridhika na nishani ya shaba katika mbio za mita 1,500 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Christchurch, New Zealand.